Searching...
Image and video hosting by TinyPic
21 December 2014
Sunday, December 21, 2014

Hatimaye Pellegrini amkamata Mourinho


Na Oscar Oscar Jr

Mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Uingereza, Manchester City jana kwenye mchezo wa mapema waliweza kuisambaratisha timu ya Crystal Palace kwa mabao 3-0 huku tofauti yao na vinara wa ligi hiyo timu ya Chelsea kubakia kuwa goli moja pekee.

Magoli mawili yaliyofungwa na kiungo mshambuliaji, David Silva na moja kutoka kwa Yaya Toure yaliwafanya wababe hao wa Uingereza kuweza kufikisha alama 39 ambazo ni sambamba na zile walizokusanya vijana wa kocha Jose Mourinho, timu ya Chelsea  ambao wakati msimu unaanza walionekana kuwa moto wa kuotea mbali.

Manchester City walikuwa na wakati mgumu mbele ya Crystal Palace hasa dakika 45 za kipindi cha kwanza na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafunga.

Dakika 45 za kipindi cha pili zilikuwa bora wa kikosi cha kocha Manuel Pellegrini huku muunganiko wa Samir Nasri, Yaya Toure na David Silva ukionekana kuwatesa walinzi wa Palace.

Kwa upande mwingine, West Ham United waliendeleza mbio zao za kujaribu kumaliza kwenye moja ya nafasi nne za juu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Leicester City na kufikisha alama 31 huku Southampton nao wakirejea kwenye ubora wao na kuwachapa Everton magoli 3-0.

Chelsea watalazimika kusubiri hadi siku ya Jumatatu ambapo watashuka dimbani majira ya saa 5:00 usiku kuwakabili Stoke City ambao mpaka sasa wana pointi 19 huku wakiwa wameshinda michezo mitano tangu kuanza kwa msimu huu. 

Ushindi kwa Chelsea utaongeza mwanya kati yao na Manchester City na kufikia kuwa alama tatu lakini matokeo tofauti na hayo, yanaweza kuongeza presha kwenye kikosi cha Chelsea ambacho kinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!