Na Chikoti Cico
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho awasifia wachezaji wanaokipiga kwenye timu mbalimbali ndani ya ligi kuu nchini Uingereza kwa kuendelea kuwa tayari kucheza kwenye kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka wakati wachezaji wa ligi zingine kama Bundesliga na La liga wakiwa mapumzikoni.
Kocha huyo Mreno kuelekea mchezo wa Chelsea dhidi ya West Ham utakaochezwa siku ya Ijumaa ambayo ni “boxing day” alisema “ni ngumu, nina heshima kubwa kwa wachezaji kwenye nchi hii, bila kujali ni Mwingereza ama sio Mwingereza. Mtu ambaye ni mchezaji wa mpira kwenye nchi hii, ninakuheshimu sana”.
“Wakati huu wachezaji Ujerumani wapo ufukweni, wachezaji wa Hispania wapo Maldives wakiota jua, kila mmoja anafanya hivyo lakini nchi hii unacheza tarehe 22 (ya Desemba), unacheza “Boxing day”, unacheza tarehe 28, unacheza siku ya mwaka mpya.
Hakuna Krismasi ni soka na nafikiri (wachezaji) wanastahili heshima”.
Pia Mourinho aliwasifia mashabiki kwa kusema “mashabiki nchini kote wanawapa hiyo heshima kwasababu kila kiwanja tiketi zimenunuliwa na nafikiri jinsi ya kufanya ni kwa namna ya weledi ambao wachezaji wangu wameonyesha”
Timu ya Chelsea ambayo Mourinho anafundisha mpaka sasa inashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 42 huku wakifuatiwa kwa karibu na timu ya Manchester City ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 39.
0 comments:
Post a Comment