Na Chikoti Cico
Manchester City na Manchester United jana jioni waliwapa mashabiki wao zawadi ya Krismasi baada ya kushinda mechi zao za ligi kuu nchini Uingereza na kuendelea kujikita kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Manchester City ambao walikuwa wageni wa West Bromwich Albion kwenye uwanja wao wa The Hawthorns walipata ushindi wa magoli 3-1 hivyo kuendelea kuifukuzia Chelsea kileleni mwa msimamo wa ligi.
Manchester City waliocheza mchezo huo bila ya washambuliaji wao watatu Aguero, Dzeko na Jovetic waliandika bao la kwanza kupitia kwa Fernando kwenye dakika ya 8 ya mchezo goli lililoiwezesha timu hiyo kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
Huku City wakiendelea kuliandama lango la West Brom kupitia kwa James Milner, David Silva na Yaya Toure vijana hao wa Manuel Pellegrini walipata goli la pili kwenye dakika ya 13 kwa njia ya penati kupitia kwa Toure baada ya Silva kuangushwa na Lescott kwenye eneo la penati.
Dakika zikiendelea kuyoyoma kuelekea mapumziko City waliandika goli la tatu kwenye dakika ya 34 kupitia kwa David Silva hivyo mpaka timu zinaenda mapumziko City walikuwa mbele kwa magoli matatu.
Kipindi cha pili ambapo sehemu kubwa ya uwanja ulijaa mvua ya “snow” kilianza kwa City kushambulia huku wakilinda magoli yao matatu lakini pia wakizidi kuendana na kasi ya mvu hiyo ya “snow” ilifunika majani ya uwanja.
Huku mchezo ukikaribia kuisha West Brom walipata goli la kufutia machozi kwenye dakika ya 87 kupitia kwa Brown Ideye baada ya kona iliyochongwa na Chris Brunt kushindwa kuokolewa vizuri na kipa wa City kabla ya Sagna kuondosha hatari hiyo na mpira kumgonga Ideye na kujaa wavuni.
Hivyo hadi mwisho wa mchezo Manchester City waliibuka na ushindi wa magoli 3-1 na hivyo kuendelea kuikaribia Chelsea kileleni kwa kufikisha alama 42.
Timu nyingine kutoka jiji la Manchester ambayo iliwapa mashabiki wao zawadi ya Krismasi ni Manchester United ambao nao pia walishinda kwa magoli 3-1 dhidi ya Newcastle United.
Newcastle walianza mchezo huo kwa kasi wakitafuta goli la mapema bila mafanikio kupitia kwa Ayole, Amstrong na Sissoko huku kikwazo kikubwa kikiwa ni beki ya Manchester na kipa wao David de Gea.
Manchester United nao walianza kulishambulia lango la Newcastle na dakika ya 23 Wayne Rooney aliipatia timu hiyo goli la kuongoza baada ya kuunganisha mpira ulioguswa na Falcao aliyepokea pasi kutoka kwa Juan Mata.
Goli hilo liliipa nguvu United na zikiwa zimebaki dakika tisa mchezo kwenda mapumziko Rooney tena aliipatia Manchester goli la pili akipokea pasi ya chini chini kutoka kwa Juan Mata hivyo hadi mapumziko matokeo yalikuwa ni 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Manchester United wakiendelea kuliandama lango la Newcastle na pasi ya umbali wa yadi 40 kutoka kwa Rooney ilimfikia Robin van Persie aliyeipatia timu hiyo goli la tatu kwa kuunganisha kwa kichwa kwenye dakika ya 53.
Newcastle walifanya mabadiliko kwa Cabela na Cisse kuingia wakichukua nafasi ya Dummett na Armstrong lakini mabadiliko haya hayakuzaa matunda huku Manchester wakiendelea kulinda magoli yao matatu.
Huku zikiwa zimebaki dakika tatu mchezo kuisha Newcastle walipata penati baada ya Colback kuangushwa na Jones kwenye eneo la hatari na Cisses kufunga penati hiyo hivyo kuwapatia vijana wa Alan Pardew goli la kufutia machozi.
Mpaka mwamuzi wa mchezo huo Mike Jones anapuliza kipenda kumaliza mchezo kwenye uwanja wa Old Trafford Manchester United walitoka uwanjani kifua mbele na kuwapa mashabiki waliofurika uwanjani zawadi ya Krismasi.
0 comments:
Post a Comment