Na Chikoti Cico
Mshambuliaji wa Liverpool, Mario Balotelli ambaye amekuwa akihusishwa kuiacha timu hiyo mapema mwezi Januari wakati wa dirisha dogo la usajili kwenye ligi kuu nchini Uingereza haondoki tena baada ya kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers kusisitiza kwamba bado anamhitaji mshambuliaji huyo.
Balotelli ambaye alisajiliwa na Liverpool toka AC Milan kwa ada ya Pauni milioni 16 ameanza kwenye kikosi cha kwanza kwenye michezo nane tu ya timu hiyo huku mpaka sasa akiwa hajafunga goli lolote kwenye michezo ya ligi.
Gazeti la Gazzetta Dello Sport la Jumamosi la nchini Italia liliandika habari ya Balotelli kutakiwa na kocha wa Inter Milan Roberto Mancini ambaye aliwahi kumfundisha mshambuliaji huyo wakati akiifundisha timu ya Manchester City.
Huku Liverpool wakiwa wanagombania makombe matatu ambayo ni EUROPA, Kombe la FA na Kombe la ligi Brendan amesisitiza kwamba hakuna mchezaji atakayeondoka kwenye timu hiyo wakati wa dirisha hilo dogo la usajili litakapofunguliwa mapema wiki ijayo.
Kuhusu habari za Balotelli kuondoka Brendan alisema “sio kitu ambacho hata nimefikiria, tuna mechi nyingi msimu huu katika mashindano mengi, katika wakati huu ni muhimu kwangu kukiweka kikosi pamoja”
Kutokuwepo kwa Daniel Sturridge ambaye ni majeruhi na ratiba ndefu ya mashindano mbalimbali inamfanya Balotelli aendelee kuhitajika kwenye timu ya Liverpool ambayo mpaka sasa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa na alama 25 baada ya mechi 18.
0 comments:
Post a Comment