Ndanda kutimua kocha tena.
Na Oscar Oscar Jr
Timu ya Ndanda ambayo imepanda daraja msimu huu, imekuwa ya kwanza kutimua kocha kati ya timu 14 zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara.
Ndanda walimtimua Kocha, Dennies Kitambi baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye michezo minne pekee huku wakishinda mchezo mmoja na kupoteza michezo mingine mitatu.
Baada ya timu kucheza mchezo mmoja chini ya kocha ambaye alikuwa mkurugenzi wa ufundi na kupoteza, Uongozi uliamua kumpa ajira Abdul Mingange kuwa kocha mkuu wa timu hiyo. Mingange alianza vema kwa kuwapatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya bingwa mtetezi, timu ya Azam.
Tayari kuna habari kuwa, Uongozi wa timu hiyo uko tayari kumlipa kocha huyo fedha zake na kusitisha ajira yake kama ataendelea kuboroga baada ya wiki iliyopita kufungwa bao 2-0 dhidi ya Ruvu Jkt ukiwa ndiyo kwanza mchezo wake wa pili tangu apewe timu.
Ndanda wameendelea kutamba kuwa, wamempa mechi nne tu za kuonyesha mabadiliko kwenye timu hiyo na akishindwa, hawaoni hasara kutafuta kocha mwingine.
Mmoja wa wakurugenzi wa timu hiyo, Mohammed Ally maarufu kama "Mamuu" amezungumza na vyombo vya habari na kusema kuwa, wamempa Mingange mechi nne tu kuhakikisha anapata matokeo mazuri lakini tofauti na hapo, watasitisha ajira yake.
Ndanda kwa sasa wanashika nafasi ya 13 wakiwa na alama sita baada ya kushinda mechi mbili na kupoteza michezo mitano. Mtibwa Sugar wanaongoza ligi hiyo wakiwa na alama 15 huku Yanga wakishika nafasi ya pili wakiwa na alama 13, sambamba na Azam wanaoshika nafasi ya tatu.
0 comments:
Post a Comment