Nani analinda kiungo na lango la Mbeya City?
Na Markus Mpangala
JUMA Mwambusi ni miongoni mwa makocha ninao wahusudu sana katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Mwingine ni Sylvester Marsh ambaye aliiwezesha Kagera Sugar kuwa moja ya timu bomb asana katika soka.
Makocha hawa wana kitu kimoja kinachofanana; kuhamasisha wachezaji wao. Juma Mwambusi naye alikuja juu ya kikosi cha mkoa wa Mbeya, na akafanikiwa kutwaa kombe la Taifa.
Baadaye sasa Mwambusi ndiye kocha wa Mbeya City kabla haijapanda Ligi Kuu Tanzania Bara. Kuna sifa nyingi sana kumhusu Mwambusi na Mbeya City. Nawafahamu Wanyakyusa kwa kasumba yao ya kupenda vya kwao.
Hawa ndiyo walionilea nikiwa shuleni jijini Mbeya na walikoleza uzalendo wangu kwa taifa. Kitu kimoja kinachoendelea sasa ni kwamba Mbeya City inashika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kinachotokea kwa Mbeya City kimenikumbusha Liverpool ya England ilivyokuwa bora msimu uliopita. Pia imenikumbusha kiwango cha Pallsons ya Arusha ilivyokuja juu kisha ikazimika ghafla.
Swali moja muhimu wanalojiuliza mashabiki na wenyeji wa jiji la Mbeya ni kitu gani kimetokea kwa Juma Mwambusi na kikosi chake cha Mbeya City? Sitazungumzia mambo ya nje ya uwanja ikiwemo kuondokewa kocha msaidizi. Nimekitazama kikosi cha Mbeya City tangu kilipopata kipigo kutoka kwa Azam fc, Mtibwa Sugar na JKT Mgambo.
Katika mechi dhidi ya Azam ilikuwa Mbeya City halisi na ilicheza vizuri kwa kiasi chake. Mambo yalikuwa mabaya zaidi kwenye mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya kuchapwa mabao 2-0 ikiwa nyumbani kwenye dimba la Sokoine.
Mechi hii natumia kama mfano, sababu ilinizindua mambo mengi mno ya kiufundi. Naweza kusema Juma Mwambusi anatakiwa kubadili mbinu haraka sana kwakuwa naamini wapinzani wake wameshafahamu namna ya kukabiliana naye. Au anatakiwa kuhakikisha Mbeya City inacheza mbinu nyingi katika mchezo mmoja.
Kwa mfano katika mechi yao na Mtibwa Sugar, hadi dakika ya 65 Mbeya City ilikuwa na ‘offside’ 1 tu wakati Mtibwa ilikuwa nazo 5. Hadi dakika ya 66 Mbeya City ilikuwa ‘shot on target’ 3 sawa na Mtibwa iliyokuwa na mashuti matatu kuelekea langoni.
Kulikuwa na mashambulizi matatu ya maana kutoka kwa Mbeya City, wakati Mtibwa ilikuwa nayo moja tu. Tofauti yake ilikuwa matumizi ya nafasi baina ya timu hizi. Ame ly alipopachika bao la Mtibwa Sugar alitumia nafasi aliyopata.
Themi Felix na Said Kipanga walikuwa na nafasi kadhaa za kufunga lakini hawakuweza kufumania nyavu. Tatizo liko wapi kwa ndugu zangu wa Mbeya City. Kocha Mwambusi anayo mbinu moja ya kukabia kwa kutumia viungo watatu.
Viungo hawa wanakuwa na jukumu la kulinda eneo la kiungo. Hassan Mwasapili alikuwa na kazi ya kucheza nafasi takribani tatu ndani ya uwanja.
Kamera za Azam Tv ziLimuonesha akiwa pembeni kulia, katikati, na pembeni kushoto. Alikuwa eneo la katikati na Steven Mazanda. Eneo la kiungo wa kushambulia anakuwa kiungo mmoja ambaye anakuwa na jukumu la kuwapikia pasi murua washambuliaji wao. Tatizo la Mbeya City dhidi ya Mtibwa walishindwa kumzidi maarifa kiungo mkongwe Shaban Nditi.
Siri ya mafnikio ya Mtibwa Sugar ipo kwa huyu kiungo mkongwe ambaye amekuwa mtulivu na ameituliza Mtibwa katika kila mechi wanayocheza. Mtibwa Sugar ina muunganiko mzuri wa safu ya ulinzi, kwahiyo kwa aina ya ushambuliaji wa Themi Felix haikuwa rahisi kupenya eneo hili.
Washambuliaji wa Mbeya City wamekuwa akicheza polepole mno, na hata wakigawana nafasi, moja kbaki eneo la hatari na mwingine kurudi nyuma kidogo wanajikuta kila mmoja anataka kufunga. Hilo ni tatizo ambalo Juma Mwambusi anatakiwa kuliona haraka.
Kiungo cha Mbeya City kinatumia wachezaji watatu kwa wakati mmoja huku kiungo mshambuliaji ni mmoja. Matokeo yake wanakosa ‘link’ kati ya kiungo wakaji kwenda kwa washambuliaji kwakuwa kiungo mshambuliaji akizidiwa maarifa basi Mbeya City imekuwa timu ya kushambuliwa.
Jambo jingine ni kwa Juma Mwambusi kuwa alitakiwa kuongeza maarifa kweye kikosi chake kwa kusajili wachezaji wapya. Mbeya City wamekaa muda mrefu pamoja.
Hii ni faida, lakini inahitaji ‘kuchaji betri’ zake ili waendelee kufaidi matunda ya kuwa pamoja. Themi Felix ameongezwa msimu huu, lakini eneo la kiungo linahitaji mchezaji mwingine mwenye ushindani zaidi ya kiwango cha Hassan Mwasapili na Steven Mazanda.
Winga Deus Kaseke anatakiwa kuendelezwa ili awe hatari kushambulia kwa kuingia ndani ya eneo la hatari kuliko kusumbua akiwa pembeni pekee.
Safu ya ulinzi inalindwa mno na viungo ambao wanatakiwa kupeleka mashambulizi lango la adui. Mwambusi anaweza kulitazama baola pili la Mtibwa, namna Vincent Barnabas alivyoweza kuwatoroka walinzi wa Mbeya City kirahisi.
Sababu Mtibwa Sugar walijua kuwa eneola kiungo lina watu wengi ambao hawajapangwa vizuri kwakuwa wanatumikia jukumu moja badala ya kuachwa kwa mchezaji mmoja.
Mpira ulivushwa eneo hilo na ukatua nje kidogo ya 18 na ikawa rahisi kwa Barnabas kuandika bao. Swali la mwisho kwa Juma Mwambusi, ameridhika na kiwnago cha golikipa wa Mbeya City? Huu ni wakati wa golikipa kuonesha ubora, vinginevyo kufanya vibaya ni ishara anahitajika kufikiri upya eneo hilo
0 comments:
Post a Comment