Na Oscar Oscar Jr
Kocha mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi tayari ameripotiwa kupeleka barua kwenye Uongozi wa timu hiyo akiomba kujiweka pembeni kuinoa timu hiyo ambayo ameiongoza kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hali hiyo imekuja baada ya timu hiyo kupoteza mwelekeo kwenye mechi saba za ligi kuu Tanzania bara ambapo timu hiyo imeshindwa kutamba.
Mwambusi amejikuta kwenye hali ngumu baada ya timu hiyo, kushinda mchezo mmoja, kutoka sare mara mbili na kuchezea kichapo mara nne na kujikuta wkishika nafasi ya mwisho (14) kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara.
Mbeya City baada ya kumaliza kwenye nafasi ya tatu msimu uliopita, watu wengi walikuwa wakiipa nafasi ya kufanya vizuri zaidi msimu huu kutokana na kupata fedha nyingi ambazo zimetokana na kuongezeka kwa wadhamini kwenye timu hiyo.
Moja kati ya sababu zinazotajwa kusababisha kocha huyo kubwaga manyanga, ni Uongozi kushindwa kutoa fedha kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye timu hiyo kama kocha alivyohitaji.
Fedha za wadhamini zimekuwa zikitolewa macho na kila kiongozi huku baadhi ya wachezaji wakiwa hawajamaliziwa fedha zao za usajili na hivyo kucheza bila ya kuwa na furaha.
Mbeya City inatajwa kuwa kwenye mgogoro wa chini kwa chini kutokana na timu hiyo kuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato na hivyo kutengeneza makundi ndani ya Uongozi mpaka kwenye timu. Kuna kila dalili kuwa, makundi hayo yamepelekea wachezaji wengi kucheza chini ya kiwango.
Bado Uongozi wa Mbeya City haujathibitisha rasmi kuziuzulu kwa kocha Mwambusi lakini ndani ya masaa 24 kila kitu kitakuwa hadharani. Moja kati ya makocha wanaotajwa kupigiwa upatu wa kuchukuwa nafasi ni pamoja na aliyekuwa kocha msaidizi wa timu ya Yanga msimu uliopita, Charles Boniphace Mkwasa.
0 comments:
Post a Comment