Jonas Mkude ni mara tano kwa Simon Msuva.
Na Oscar Oscar Jr
Ndivyo unavyoweza kusema kwa lugha rahisi kuwa, kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga, Simon Msuva kwa sasa anauzwa mara tano ya gharama ya kumpata Jonas Mkude. Dirisha la usajili limefunguliwa jana ligi kuu Tanzania bara na habari kubwa ni Msuva kutakiwa na klabu ya Simba.
Kiungo wa Simba, Jonas Mkude ni moja kati ya wachezaji walioanza kutikisa dirisha hili la usajili na baadaye Simba wakafanikiwa kumuongeza mkataba wa miaka miwili kwa kiasi cha fedha kilichotajwa kuwa ni shilingi Milioni 60.
Klabu ya Yanga ni moja kati ya timu ambazo zilikuwa zinamuwania mchezaji huyo kwa karibu sana kutokana na kumpoteza mwishoni mwa msimu uliopita kiungo, Frank Domayo amabaye alijiunga na mabingwa wa msimu huo, timu ya Azam.
Simon Msuva anahitajika kwenye klabu ya Simba kwa udi na uvumba lakini, dau lake limekuwa likipanda kila jua linavyochomoza.
Wakati Uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wake wa kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope ukitangaza kumuhitaji mchezaji huyo, Yanga walidai kuwa hawana tatizo lakini uhamisho huo utawalazimu Simba kulipa Milioni 200.
Msuva ni moja kati ya wachezaji wachache sana kwenye kikosi cha Yanga walionyesha uwezo wa juu msimu huu huku akiwa mfungaji bora wa klabu yake kwa kufunga mabao matatu kwenye michezo saba iliyokwishapigwa hadi sasa licha ya kuwa mchezaji huyo amekuwa akitokea benchi.
Habari zilizotoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari leo, zimedai kuwa Yanga wameongeza dau kwa yoyote atakaye mtaka kiungo huyo, atalazimika kulipa Milioni 300.
Kama Simba watalipa fedha hizo na kumchukuwa, bei hiyo itakuwa mara tano ya kiasi kilichotumika kumsainisha mkataba mpya kiungo, Jonas Mkude.
0 comments:
Post a Comment