Na Chikoti Cico
Msimu uliopita wa ligi kuu nchini Uingereza Manchester City walikuwa bora karibu kila idara na Etihad palikuwa ni machinjioni kwa timu nyingi zilizocheza pale na City, unaweza kusema katika msimu ambao fedha za Shekh Mansour zilionekana kufanya kazi basi ni msimu uliopita kwani waliweza kuchukua makombe mawili la Barclays na Capital one huku wakifika kwa mara ya kwanza hatua ya mtoano kwenye ligi ya mabingwa Ulaya.
Umewaona Manchester City wa msimu huu kwa haraka haraka ni ngumu kuamini kama hawa ni mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Uingereza, ni ngumu kuamini kwamba hii ni timu ambayo ilifunga magoli 102 msimu uliopita na kumaliza ligi ikiwa na alama 86, mpaka sasa City ya msimu huu inaonekana kupotea na haifanani na ile City ya msimu uliopita.
Hebu tuangalie nini kinawasibu Manchester City ambao wameshatolewa kwenye kombe la Capital One na pia wana nafasi finyu ya kuvuka kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Ulaya kwani mpaka sasa City wanashika mkia kwenye kundi E wakiwa na alama mbili huku akiwa amebakiza mechi mbili dhidi ya Bayern Munich na Roma.
Sababu ya kwanza inayoweza kuwa inawasibu City ni uchovu (fatigue) hii ni baada ya kutumia nguvu nyingi sana kwenye msimu uliopita kuutafuta ubingwa, ukiangalia mpaka dakika za mwisho walikuwa wanakimbizana na Liverpool na Chelsea kuwania ubingwa wa ligi na mpaka wanachukua ubingwa walipishana kwa alama mbili na Liverpool na alama nne na Chelsea hivyo haikuwa kazi rahisi.
Sababu ya pili ni kumtegemea sana Yaya Toure ukiangalia kwenye msimu uliopita Manchester City walimtegemea sana Toure kuamua matokeo ya mechi nyingi na mpaka msimu unaisha, alichangia magoli 29 ambapo alifunga magoli 20 na kutoa pasi tisa za magoli lakini toka kuanza kwa msimu huu Toure bado hajawa kwenye kiwango kama cha msimu uliopita na hii imepelekea City kuyumba.
Pamoja na kwamba yeye ndiyo suluhisho la kuyumba kwa City lakini pia yeye mwenyewe ni tatizo hapa namwongelea kocha Manuel Pellegrini, huyu ni kocha anayependa kucheza na washambuliaji wawili bila kuangalia mpinzani ana ubora kiasi gani hasa kwenye eneo la katikati ya uwanja.
Ukiangalia mechi za City dhidi ya Bayern Munich tokea msimu uliopita wa ligi ya mabingwa Ulaya City walifia katikati ya uwanja hivyo matokeo mabovu ya UEFA mengine ni kwasababu ya kosa hili.
Pia ukiangalia wastani wa umri wa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Manchester City ni mkubwa ukilinganisha na timu zote kwenye ligi ya Uingereza, kikosi cha kwanza cha City kina wastani wa miaka 28.5 hii inamaanisha kikosi cha wachezaji wa City hakiwezi kuwa na kasi ile ile kama ya msimu uliopita na ni ngumu kukimbia kilomita nyingi uwanjani na kupata matokeo kirahisi.
Pamoja na sababu zote hizo zinazoonyesha mambo ambayo inawezekana ndiyo yanayowasibu Manchester City kwasasa, bado naamini City wataamka na kurejea kwenye makali yao kwa jinsi ligi inavyozidi kuchanganyia ila kwa upande wa ligi ya mabingwa Ulaya City wana kazi kubwa zaidi ili kuvuka hatua ya makundi.
Chukua hii: Kila Manchester City wanapoingia (qualify) kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya Yaya Toure huwa anaweka kibindoni paundi 823,000 kama bonasi.
NAWASILISHA.
0 comments:
Post a Comment