Azam vs Coastal Union Jumamosi hii.
Na Oscar Oscar Jr
Siku ya Jumamosi itapigwa moja ya mechi ambayo kwa mpenda soka la nyumbani, hatotamani kuikosa. Katika viwanja vya Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kutakuwa na mchezo utakao wakutanisha Azam Fc dhidi ya Coastal Union kutoka mkoani Tanga.
Azam wametoka kupoteza mechi mbili mfululizo baada ya kufungwa weekend iliyopita na timu ya Ndanda Fc kabla ya hapo awali kupoteza mchezo wao dhidi ya Ruvu JKT.
Rekodi ya Coastal Union inaonekana kuimarika kadiri siku zinavyokwenda mbele, wameshida michezo mitatu na kufunga jumla ya magoli nane huku akipoteza mchezo mmoja pekee na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Mtibwa Sugar.
Didier Kavumbagu wa Azam, ndiyo mshambuliaji aliyebeba matumaini makubwa kutika kuzifumania nyavu za wapinzania baada ya John Bocco na Kipre Tchetche kuwa nje kwa sababu mbalimbali.
Kumkosa Kipre Tchetche kwenye michezo miwili iliyopita, Azam wamejikuta wakipoteza mechi hizo lakini bila shaka kurejea kwa mshambuliaji Lionel Saint Preux aliyekuwa majeruhi, kutaongeza nguvu kikosini huku Kavumbagu akitarajiwa kurejea kwenye ufungaji baada ya kujikuta akiganda na magoli yake manne.
Azam wako kwenye nafasi ya tatu baada ya kushuka dimbani mara sita na kujikusanyia alama 10 ambazo ni sawa na walizopata timu ya Yanga inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu.
Coastal Union walianza ligi huku wakiwa na migogoro ya Uongozi lakini kwa sasa, wanaonekana kutulia na timu inazidi kufanya vizuri. Pamoja na kuonekana Coastal Union wako vizuri, safu yao ya ulinzi tayari imesharuhusu kufungwa magoli matano.
Ukata wa Coastal Union utakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wa wanalamba lamba hao ambao mpaka sasa, wamefunga jumla ya mabao sita ambayo ni wastani wa goli moja kwenye kila mchezo.
Ushindi kwa upande wa Coastal Union, utawafanya kijiweka kwenye mazingira mazuri ya mbio hizo za ubingwa huku kipigo kwa Azam, kitapokelewa kwa simanzi kubwa hasa ukizingatia wamepoteza mechi mbili mfululizo.
Azam wanahitaji kushinda mchezo huo ili kujiweka vizuri kuelekea kutetea Ubingwa wao na kuhakikisha wanarejesha hali ya kujiamini kwani baada ya mechi ya Jumamosi hii, watakuwa wanajiandaa kuwavaa Yanga kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment