Na Chikoti Cico
Mchezaji bora wa dunia mara nne, Lionel Messi afikia rekodi ya mchezaji wa zamani wa Real Madrid na Schalke 04, Raul Gonzalez ya magoli 71 ya ligi ya mabingwa Ulaya.
Messi amefikia rekodi hiyo baada ya kufunga magoli mawili ya ushindi kwa timu ya Barcelona dhidi ya Ajax katika mchezo wa kundi F kwenye mzunguko wa pili wa ligi ya mabingwa Ulaya uliochezwa usiku wa Jumatano.
Messi amefanikiwa kufikia rekodi hiyo akimpita mshambuliaji wa Real Madrid na mchezaji bora wa dunia kwa mwaka jana, Christiano Ronaldo mwenye magoli 70 ambaye alishindwa kufikia ama kuivunja rekodi hiyo kwenye mchezo dhidi ya Liverpool baada ya kutoka bila kufunga goli lolote.
Messi na Ronaldo ambao wanatajwa kuwa ni moja ya wachezaji bora na mahiri kwasasa duniani huku wakihusika kufikia na kuvunja rekodi mbalimbali za magoli, wana nafasi kubwa ya kuweza kuvunja pia rekodi hiyo ya Raul na hata kuweka rekodi mpya ya magoli mengi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya.
Messi ameweza kufikia rekodi hiyo ya magoli 71 baada ya kucheza michezo 90 ya ligi ya mabingwa Ulaya akiwa na timu ya Barcelona na kufanikiwa kunyakua kombe la ligi ya mabingwa Ulaya mara tatu wakati Raul Gonzalez, ilimchukua michezo 142 kuweza kuiweka rekodi hiyo.
Ronaldo ambaye ana magoli 70 ya michuano hiyo, anaendelea kusalia kwenye nafasi ya tatu huku Messi na Gonzalez wakiwa wamefungana kwa kila mmoja kufikisha magoli 71.
Kupitia Ushindi wa jana, Barcelona wamejihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ambayo bingwa wake mtetezi ni klabu ya Real Madrid.
0 comments:
Post a Comment