Na Oscar Oscar Jr
Timu ya Yanga ambayo ilikuwa imeweka kambi kwenye mji wa Kahama, leo imeshuka dimbani kupambana na timu ya Ambassador fc ya Kahama na kufanikiwa kushinda bao 1-0 goli lililofungwa na mshambuliaji Said Bahanuzi.
Yanga wameweka kambi Kahama huku wakijiandaa na mchezo wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa dimba la Kaitaba Jumamosi hii.
Katika mchezo wa leo, kocha wa Yanga Marcio Maximo aliamua kuanzisha kikosi ambacho wachezaji wake mara kadhaa hutumika wakitokea benchi.
Pamoja na kuwepo malalamiko ya Meneja wa mchezaji, Juma Kasseja akimtaka kocha Maximo amtumie kipa huyo, bado Maximo ameendelea kumtumia kwenye mechi za kirafiki pekee.
Baada ya kupata ushindi huo, Yanga watakuwa wanajiandaa kuelekea mkoa wa Kagera kwenda kupambana na kuhakikisha wanaibuka na alama tatu.
Yanga wako kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu bara na hiyo ni baada ya kujikusanyia alama 10 ambazo ni sawa na timu ya Azam na kinachowatofautisha ni uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa.
0 comments:
Post a Comment