Na Oscar Oscar Jr
Vinara wa ligi kuu nchini Hispania, timu ya Barcelona watashuka dimbani leo kucheza na timu SD Eibar majira ya saa 3:00 usiku. Mchezo utapigwa pale Nou Camp baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa kumalizika.
Barcelona ya msimu huu, inaonekana kuimarika mno hususani kwenye safu yao ya Ulinzi inayoongozwa na golikipa Claudio Bravo na hadi sasa, hawajaruhusu nyavu za goli lao kutikiswa hata kwa bao moja.
Ujio wa Ivan Rakitic na ubora wa Andres Iniesta, umeifanya Barcelona kuimarika kwenye safu ya kiungo huku Lionel Messi na Neymar Jr wakicheka na nyavu za wapinzani kila kukicha.
Barcelona wataingia kwenye mchezo wa leo wakiwa kwenye nafasi ya kwanza baada ya kushinda michezo sita na kutoka sare mmoja na kuwafanya kujikusanyia alama 19 huku, Eibar wako kwenye nafasi ya tisa baada ya kushuka dimbani mara saba.
SD Eibar ni timu ambayo haipewi nafasi kubwa sana ya kushinda kwenye mchezo wa leo lakini, unapotazama safu yake ya ulinzi unapaswa kuwaheshimu.
Eibar Wanashika nafasi ya tatu kwenye La Liga kama timu yenye safu bora ya ulinzi na hii ni baada ya wao kuruhusu mabao saba tu huku Valencia, wakiruhusu manne na Barcelona ambayo haijaruhusu hata moja.
Barcelona anahitaji kushinda leo ili kuendeleza rekodi yake ya kutofungwa msimu huu kwenye La Liga huku, akihitaji pia kushinda mchezo wake wa ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Ajax kabla ya kuwavaa Real Madrid mwishoni mwa juma lijalo kwenye mchezo wa El-Classico.
Katika michezo miwili ya ugenini msimu huu, Eibar wameshinda mmoja na kutoka sare michezo yote bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
Hii ni mechi ambayo ina zikutanisha timu mbili zenye safu bora za ulinzi lakini, Lionel Messi ndiye mchezaji anayeongoza mpaka sasa kwenye ligi hiyo kwa kupiga pasi nyingi za zilizozaa magoli (6) ni wazi kuwa, atawasumbua sana Eibar usiku wa leo.
Kikosi cha Barcelona kinachoweza kuanza (4-3-3): Bravo; Alves, Piqué, Mascherano, Adriano; Busquets, Xavi, Rakitić; Pedro, Messi, Munir
Kikosi cha Eibar kinachoweza kuanza (4-2-3-1): Irureta; Boveda, Navas, Albentosa, Abraham; Errasti, Garcia; Lara, Piovaccari, Saul; Angel
0 comments:
Post a Comment