NIONAVYO MIMI: NASUBIRI MAANDISHI MAPYA YA BALOTELLI.
Na Oscar Oscar Jr
Ni miaka mitatu sasa imepita tangu Super Mario Balotelli alipoifunga Manchester United na kisha kuvua T-Shirt iliyokuwa na maandishi ya " Why always me?" lakini mpaka leo, bado mashabiki wa soka wanakumbuka tukio hilo. Unaanzia wapi kusahau tukio kama lile? Huwezi hata siku moja.
Upo uwezekano watu wakawa wamesahau Hat-trick iliyofungwa na mshambuliaji wa chelsea Andre Schurrle kwenye mchezo dhidi ya Fulham msimu uliopita lakini, ni vigumu kusahau goli moja alilofunga Demba Ba kwenye mechi ya Chelsea dhidi ya Liverpool kule Anfield.
Unajua kwa nini? goli moja unalofunga dhidi ya Manchester United, Manchester City, Arsenal, Chelsea au Liverpool, linatawala akili za watu kwa muda mrefu kuliko Hat-trick mchezaji anayofunga dhidi ya Leicester City au Burnley.
Msimu uliopita Liverpool ilifungwa mabao mengi (50) kuliko timu yoyote iliyomaliza ndani ya nne bora na hata Manchester United pamoja na kumaliza kwenye nafasi ya saba, bado hawakuruhusu mabao mengi kama ilivyokuwa kwa Liverpool.
Ukiondoa Manchester City waliotwaa ubingwa, hakuna timu nyingine iliyofunga magoli mengi kuizidi Liverpool. Nguvu ya Liverpool, iko kwenye safu ya ushambuliaji.
Tayari wamempoteza Luis Suarez aliyejiunga na klabu ya Barcelona baada ya kuifungia Liverpool magoli 31 na kupika mengine 14 msimu uliopita akiwa na Majogoo hao wa Jiji la Liverpool. Kurejea kwa Daniel Sturridge, kuna weza kuleta tumaini jipya kwa timu hiyo.
Sifa kubwa ya mshambuliaji ni kufunga magoli na kwa bahati mbaya, Mario Balotelli hana rekodi nzuri katika hilo. Unapokuwa na timu kama Liverpool yenye kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi, unahitaji kuwa na washambuliaji wenye uwezo wa kufunga zaidi ili uweze kufanikiwa. Balotelli hajawahi kufunga zaidi ya magoli 14 za ligi kuu katika maisha yake ya soka.
Wakati Sturridge akifunga mabao 21 na kutengeneza mengine saba msimu uliopita, Balotelli akiwa na Manchester City kwa misimu yote miwili na nusu, amefunga mabao 20 tu na kutengeneza moja pekee. Unakumbuka bao lenyewe alilotengeneza?
Ilikuwa ni pasi kwenye dakika ya 94 aliyompatia Sergio Aguero kwenye mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya QPR na bao hilo likawapatia ushindi wa taji la ligi kuu ambalo mashabiki wa Etihad walilikosa kwa zaidi ya miaka 40. Hii pasi ya mwisho kutoka kwa Balotelli kwenda kwa Aguero huwezi kuisahau hata kidogo.
Pamoja na kuwa hajafunga bao lolote la EPL akiwa na Liverpool, tayari Balotelli ameshabadilisha rangi na style yake ya nywele mara moja na kuvua bukta yake huku akibaki na nguo ya ndani kwenye uwanja wa mazoezi mara moja pia. Unamjua Balotelli au Unamsikia?
Bado Liverpool haijakutana na Chelsea, Arsenal wala Manchester United. Hizi ndiyo aina ya mechi ambazo Super Mario huwa zinamuweka mjini.
Hizi ndiyo mechi ambazo huwa anakuja na maandisha mapya kwenye flana yake ya ndani. Bila shaka awamu hii, anaweza kuvua hata bukta yake.
Bado naamini Mario atafunga lakini sioni uwezekano wa yeye kufunga zaidi ya mabao 15 msimu huu. Mabao yake mengi yamefungwa kwenye mechi kubwa na kusindikizwa na vituko vyake.
Olivier Giroud na Romeru Lukaku, wanarekodi nzuri ya mabao EPL kuliko Super Mario lakini ukubwa wa jina la Balotelli ni zaidi ya hao wote. Ngoja niendelee kusubiri maandishi mapya ya flana yake ya ndani.
0 comments:
Post a Comment