NIONAVYO MIMI: NADIR HAROUB NI KAMA BABA MWENYE NYUMBA.
Na Oscar Oscar Jr
Kuna muda unarudi nyumbani saa mbili usiku kutoka kwenye mizunguko yako ya kutwa nzima huku mfukoni ukiwa huna hata shilingi mia tano. Unasikikitika lakini siku inakuwa ndiyo imekwisha hivyo.
Unapomueleza mwenzi wako kuwa hukupata chochote, anaweza kukuelewa lakini panavyokaribia kucha, anakuuliza " Kwa hiyo leo tunaishije"? usisikitike sana unapoulizwa swali kama hili. Unapokuwa baba mwenye nyumba, unatakiwa kuonyesha njia hata kama mazingira ni magumu kiasi gani.
Nahodha wa Taifa Stars Nadir Haroub maarufu kama Canavaro, anaonyesha njia kama baba wa Taifa Stars kila awapo uwanjani. Kupanga na kuiongoza safu ya ulinzi ya timu hiyo ni jukumu lake la msingi na kusaidia mashambulizi, ni jukumu lake la ziada. Hakuna ubishi, anatimiza haya yote kwenye timu ya taifa na kwenye klabu yake ya Yanga.
Baba mwenye nyumba hatakiwi kuyumba moja kwa moja. Anaweza kuyumba kwa masaa kadhaa kisha, akarejea kwenye ubora wake na kuiongoza familia.
Msimu wa 2012/2013 pamoja na Yanga kutwaa ubingwa, Nadir Haroub hakuwa kwenye kiwango kizuri. Tangu kuanza kwa msimu wa 2013/2014 hadi leo, Nadir amekuwa baba mwenye nyumba, kila kukicha anazidi kuimarika.
Msimu uliopita akiwa na klabu yake, alifunga bao zuri na kuipatia ushindi Yanga mbele ya Al Ahly ya Misri mechi ya kwanza jijini Dar es salaam. Alionyesha njia pia kwenye mechi za awali kufuzu AFCON Morocco mwakani pale alipofunga bao ugenini dhidi ya Zimbabwe na kuifanya Taifa Stars kutinga hatua ya pili ya mchujo.
Jana pia, alionyesha kuwa yeye ndiye baba mwenye nyumba kwa kufungua akaunti ya mabao pale alipofunga bao la kwanza dhidi ya Benin na kuifanya Stars ishinde kwa bao 4-1.
Mabadiliko ya kumtoa Cannavaro na kumuingiza Said Morad kwenye dakika ya 75 kwenye mechi dhidi ya Benin, ilikuwa ni kwa sababu aliumia lakini nadhani kitaalamu, inapaswa kuwa hivyo.
Ni muda sahihi kwa sasa kumpunguzia dakika za kucheza uwanjani kwenye timu ya taifa na hata kwenye klabu yake ili kupata kilicho bora kutoka kwake.
Pamoja na mazuri mengi kutoka kwake, Cannavaro ni binadamu. Umri unakwenda, nguvu zinapungua na ubora utapotea kabisa. Akipunguziwa muda wa kucheza, anaweza kudumu kwa muda mrefu.
Kelele anazopigiwa Steven Gerrard wa Uingereza, kelele anazopigiwa Iker Cassilas wa Hispania, nisingependa zimkute Nadir. Nisingepende kuona zinamkuta nahodha wetu wa Stars.
Steven Gerrard alikuwa baba bora wa England na Liverpool lakini, muda ni ukuta. Iker Casillas amekuwa nahodha bora wa Real Madrid na Hispania lakini kwa sasa, mambo si mambo.
Jose Mourinho aliwastua mapema Real Madrid lakini alipoondoka tu, wakaendelea kulala na kumkumbatia. Gerrard alipima mwenyewe na akaamua kustaafu soka la kimataifa.
Liverpool bado wanamuonea aibu lakini kitendo cha kocha Brendan Rodgers kumteua Jordan Henderson kuwa nahodha msaidizi, ni wazi kuwa anajiandaa kuijenga Liverpool mpya bila Gerrard.
Kuna habari kuwa kipa David De Gea anajiandaa kuchukuwa nafasi ya Cassilas, sio mbaya ingawa wamechelewa. Walipaswa kuanza kumtumia kabla hata ya kombe la Dunia kule Brazil.
Nadir anapaswa kutafutiwa mbadala wake kwenye klabu na timu ya Taifa. Tusimpe sifa kisha tusubiri mpaka atakapoanza kuanguka kama ilivyokuwa kwa Gerrard kwenye mechi na Chelsea pale Anfield msimu uliopita.
Mecky Mexime, Shedrack Nsajigwa na manahodha wengine, walifanya kazi nzuri sana ya kuipeperusha bendera ya taifa ya Tanzania na kwa sasa, Nadir inaifanya kazi hiyo.
Kama kocha Marts Nooij ana amini kuwa Nadir ataendelea kuwa kwenye ubora ule ule kwa kucheza dakika zote 90 kwa miaka mingine mitatu, itabidi nimnunulie miwani mingine ya kumtazamia Nadir Haroub.
0 comments:
Post a Comment