Ni muda wa kocha Maximo kumtazama upya Jerryson Tegete.
Na Samuel Samuel
Mshangao wangu ulianza toka mechi iliyopigwa pale uwanja wa taifa baina ya JKT Ruvu na Yanga na baadae, tarehe 18 baina ya Simba SC na Yanga.
Katika lundo la washambuliaji wa kati waliopo pale Jangwani, kwa sasa Tegete ndiye mchezaji aliyeifungia Yanga magoli mengi zaidi na mkongwe katika nafasi hiyo.
Ikumbukwe toka akiwa na miaka 19 akitokea pale Makongo Sec, Tegete hajawahi kuhama timu hiyo na kabla ya kuja Kavumbagu, Bahanuzi, Javu na Jaja.
Tegete alikuwa moto wa kuotea mbali akitengenezewa mipira mizuri na viungo kama Chuji, Domayo, Nizar na Haruna Niyonzima. Maximo toka mwanzo wa ligi ilimpasa kumpa si chini ya dakika arobaini mchezaji huyu.
Tegete ni mmoja wa washambuliaji hatari sana nchini kwa kuzitendea haki pasi za mwisho. Ana uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya huu na chini kitu ambacho ni nadra kwa washambuliaji wengine.
Nilisema pale Mwanzo sishangazwi na alichokifanya Tegete pale Shinyanga kwa sababu, ndicho sikuzote natarajia akifanye pale jezi namba kumi inapong'ara mgongoni mwake.
Amekuwa na uwezo mzuri akipewa nafasi hasa kwenye viwanja vibofu vya mikoani. Ikumbukwe ni kombinesheni hiyo hiyo aliyoitumia juzi Maximo ya kumuweka Javu na Tegete msimu uliopita iliwashusha Rhino kwenye ligi pale uwanja wa Alhassan Mwinyi mkoani Tabora.
Yanga ilishinda 3-0 Tegete akifunga goli la pili. Maximo anatakiwa agundue saikolojia ya mchezaji huyu. Tegete anahitaji kupata mechi nyingi ili acheze kwa sababu ni mchezaji ambaye akikosa majukumu mazito kwenye timu huanza kujisahau na starehe au kutofanya mazoezi kwa bidii.
Katika umri wa miaka 26 aliyonayo, bado ana muda mrefu wa kuonesha kipaji chake na kuisaidia Yanga. Kama alivyoanza kumtumia ndivyo hivyo hivyo aendelee kumpa nafasi ili kumrudisha mchezoni kisaikolojia na kumpa hamu ya kucheza.
0 comments:
Post a Comment