Searching...
Image and video hosting by TinyPic
18 October 2014
Saturday, October 18, 2014

Kuelekea Yanga vs Simba leo pale Taifa.





Na Oscar Oscar Jr


Mchezo wa Yanga na Simba siku zote ni zaidi ya alama tatu wanazogombea ndani ya dakika 90. Huu ni mchezo wa kutengeneza heshima kwa viongozi, wachezaji, makocha na mashabiki wa soka katika nchi hii. Kushinda mchezo wa leo unapokelewa kwa shangwe na wahusika, kuliko hata kushinda taji la ligi kuu.

Wakati Simba hawapewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri, wamekuwa wakicheza vizuri sana na kuwazuia Yanga. Hii ni mechi nyingine ambayo Yanga anapewa nafasi kubwa ya Kushinda kutokana na matokeo aliyonayo mpaka sasa na uwepo wa wachezaji wake wote tegemeo. 

Pamoja na kuwa Simba haikuanza ligi vizuri, majeruhu ya baadhi ya wachezaji wake muhimu yameendelea kuwagharimu.

Kuna habari za kuumia kwa magolikipa wote wawili wa timu hiyo ya Msimbazi ingawa, inadaiwa kuwa Ivo Mapunda amepata nafuu na atakuwa tayari kucheza mchezo wa leo. 

Goli kipa ni mchezaji muhimu sana kwa sababu, anacheza mahali panapoamua hatima ya mchezo. Kutokuwa fiti kwa asilimia mia moja kwa mchezaji wa eneo hilo, kunaweza kuigharimu Simba.

Safu ya Ulinzi ya Simba ambayo inaongozwa na Joseph Owino, tayari imesharuhusu magoli manne mpaka sasa lakini, bado sioni tatizo kubwa sana kuelekea mchezo wa leo kama Said Ndemla, Kwizerra na Jonas Mkude wataifanya kazi yao vema kwenye eneo la kiungo la timu hiyo.

Njia nzuri ya kumzuia mpinzani wako ni kutompa nafasi ya kumiliki mpira. Simba inaundwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa kumiliki mpira na kama hili litafanikiwa, basi wanaweza kuwa na mchezo mzuri siku hii ya leo. Ramadhani Singano, Amri Kiemba na Emmanuel Okwi, wanajua namna ya kukaa na mpira.

Aina ya mpira wanaocheza Yanga msimu huu, sio wa kufunga magoli mengi na hasa pale wao wanapotangulia kupata goli. Yanga wanatumia viungo wengi huku wakimuacha mshambuliaji mmoja pekee ingawa kwenye mchezo kama wa leo, kocha anaweza kuja na mbinu tofauti kabisa. 

Simoni Msuvu na Mrisho Ngassa wamekuwa hawaanzi pamoja kitu kinachofanya Yanga iwe bora kwenye winga moja karibu kwenye kla mchezo waliocheza msimu huu.

Nadhani Msuva na Ngassa wanapaswa kuanza kwenye mechi ya leo ili kutumia faida ya kasi waliyonayo  wachezaji hawa kufunga magoli pindi Simba watakapopoteza Mpira. 

Ni kweli Simba wana watu wa kuchezea mpira wengi lakini ni wazi kuwa, Yanga inawachezaji wenye kasi kuliko Simba.

Deogratius Munishi kipa wa Yanga, alifungwa goli zuri sana dhidi ya JKT Ruvu na mchezaji Jabir Azizi kwa mkwaju mkali wa mbali. Leo hii Dida anatakiwa kuwa makini muda wote kwani Jonas Mkude na Amri Kiemba kama wataanza, wanauwezo mkubwa wa  kupiga mikwaju hiyo.

Namna anavyocheza Mbuyu Twite kama kiungo mkabaji, kuna muda inaonekana kama Yanga wanacheza na walinzi watatu wa kati. Mbuyu Twite, Kelvin Yondani na Nadir Haroub wote wanakuwa sawa kitu ambacho wanaweza kupigwa chenga moja wote watatu. 

Nadhani Twite anapaswa kusogea kwa juu kidogo ili kama anapitwa basi, Yondani na Nadir wawe na nafasi nyingine ya kumlinda Dida.

Jaja na Okwi pengine ndiyo wanazungumzwa sana kwenye mchezo huu. Okwi tayari anagoli moja na kahusika kwenye magoli mengine mawili ya Simba msimu huu huku Jaja pamoja na kucheza vizuri, bado hajafanya makubwa. 

Mchezo huu unaweza kuwa wa Haruna Niyonzima dhidi ya Amri Kiemba au Harouna Chanongo dhidi ya Simoni Msuva. Nani kuibuka kidedea? Tukutane uwanja wa Taifa.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!