Daley Blind anataka kucheza kiungo pale Man United
Na Oscar Oscar Jr
Kijana mpya wa Manchester United, Daley Blind, ametangaza kuwa angependelea kucheza kwenye dimba la kati la timu hiyo yenye maskani yake kwenye dimba la Old Trafford kama alivyokuwa anatumiwa na meneja wake wa zamani pale Ajax Amsterdam, Frank de Boer.
Blind, 24, alishinda mataji manne ya ligi kuu ya Uholanzi, Eredivisie, chini ya De Boer akichezea Ajax kama kiungo mwenye uwezo wa kubadilisha nafasi ya kucheza kabla ya kukamilisha uhamisho wa pauni milioni 14 wa kutua Old Trafford mwezi uliopita.
Blind alitumika muda mrefu kama beki wa kushoto kwenye Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Uholanzi chini ya meneja wake mpya United, Louis Van Gaal, lakini anaweza kucheza upande wa kushoto na kiungo cha kati.
Pamoja na kuonyesha mapungufu makubwa kwenye safu ya kiungo na ulinzi, Manchester United bado haionekani kufanya vizuri kwenye safu ya ushambuliaji ambapo mpaka sasa wamefunga mabao mawili pekee na kuruhusu wavu wao kutikiswa mara tatu.
Ujio wa winga na kiungo mshambuliaji Angel Di Maria na mshambuliaji Radamel Falcao kunaleta matumaini makubwa kwa wababe hao wa ligi kuu ya Uingereza, kuimarika kwenye safu ya ushambuliaji. United wanatarajia kuvaana na QPR kwenye mzunguko wa nne wa ligi hiyo.
0 comments:
Post a Comment