Searching...
Image and video hosting by TinyPic
15 August 2014
Friday, August 15, 2014

Sitashangaa Diego Costa akimpa Jose Mourinho taji la EPL



 Na Chicoti jr (Cico cicod)

 Tarehe 13 ya Mwezi wa Aprili 2014 Atlectico Madrid walicheza dhidi ya Getafe kwenye ligi ya Hispania maarufu “la liga” na Atletico Madrid kushinda kwa goli 2-0 huku goli la pili likifungwa na Diego Costa goli lililosababisha Costa kugonga nguzo ya goli na mguu kuchanika, kocha wa Atletico Madrid , Diego Simone alipoulizwa vipi Costa anaendeleaje alisema “yuko sawa, mkwaruzo hauwezi kumuumiza chui” maneno hayo machache yanakupa picha ya upiganaji wa Diego Costa anapokuwa uwanjani. 

Baada ya kuipa ubingwa wa la liga timu ya Atlectico Madrid huku akifunga jumla ya magoli 27 na kuifikisha fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya (UEFA) Diego Costa amesajiliwa na Chelsea ya Uingereza hivyo kwa msimu wa 2014/2015 Costa atavalia jezi za bluu kuongoza safu ya ushambuliaji ya Chelsea chini ya kocha Jose Mourinho, safu ambayo kwa msimu uliopita ilikosa makali na kupelekea Mourinho kushindwa kupata kombe lolote. 

Ukimwangalia Costa ni aina ya washambuliaji ambao kocha Jose Mourinho amekuwa akipenda kufanya nao kazi, wakati akiwa kocha wa Porto safu ya ushambuliaji iliongozwa na Benni McCarthy na kupelekea kufanikiwa kuchukua kombe la ligi ya Ureno na kunyakuwa ubingwa wa UEFA huku McCarthy akiibuka mfungaji bora. 

Aliposajiliwa kuifundisha Chelsea mwaka 2004 Mourinho alimsajili Didier Drogba kutoka Olympique de Marseille na kufanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi ya Uingereza kwa misimu miwili mfululizo huku Drogba akiifungia Chelsea jumla ya magoli 32.

Alipokwenda kuifundisha Inter Milan ya Italia Mourinho alimsajili Diego Milito kutoka Genoa na hatimaye kuchukua makombe matatu (treble) huku Milito akifunga jumla ya magoli 30.

Katika umri wa miaka 25 ni dhahiri Costa yuko katika umri ambao bado anahamu ya mafanikio, hamu ya kutaka kushinda vikombe vingi zaidi hasa ubingwa wa UEFA alioukosa mwaka jana na zaidi kujitengenezea mazingira mazuri zaidi kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu ya taifa ya Hispania.

Pamoja na kwamba ligi ya Uingereza huwa inamchukua muda kwa wachezaji kutoka ligi zingine kuizoea lakini kwa aina ya uchezaji wa Costa haitamchukua muda mrefu kwasababu ni mshambuliaji ambaye anaweza kusimama peke yake na kufunga lakini pia utumiaji wa nguvu kwenye ligi ya Uingereza hautampa wakati mgumu kwasababu ni aina ya washambuliaji ambao wanajulikana kwa matumizi ya nguvu uwanjani.

Pamoja na kwamba kuna washambuliaji ambao hawakung’ara kipindi cha Mourinho toka 2004-2007 kama Adrian Mutu, Hernan Crespo, Mateja Kezman na Andriy Shevchenko ila bado Diego Costa anabaki kuwa mshambuliaji ambaye atafanya makubwa kwasababu hana presha ya kupokonywa namba huku usajili wa Didier Drogba ukionekana utatoa changamoto ndogo kwa Costa lakini zaidi Fernando Torres bado hajarudi kwenye kiwango cha kumweka benchi Costa.

Safu ya ushambuliaji ya Chelsea zaidi ya kuwa na Diego Costa bado kuna viungo wenye kuiongezea makali, wachezaji kama Fabregas, Hazard, Oscar na Willian wote kwa pamoja watakuwa na kazi ya kurahisisha ufungaji wa Costa lakini pia kuifanya Chelsea ing’are kwa msimu mpya wa ligi ya EPL na kufanikiwa kuchukua ubingwa baada ya kuupoteza toka 2010.

NAWASILISHA @

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!