Searching...
Image and video hosting by TinyPic
13 August 2014
Wednesday, August 13, 2014

Ni muda wa kocha wa Azam kutimiza ndoto za mabosi wake.



Na ABUU HOZZA.

Joseph Omog ana jukumu la kuifanya Azam Fc itawale Afrika. Azam fc tayari wamekamilisha ndoto yao ya muda mrefu ya kushinda taji la ligi kuu Tanzania bara kwa mamilioni ya pesa ambayo makampuni ya SBS yamewekeza katika timu hiyo walistahili kushinda kombe hili.

Wamevunja utawala wa muda merfu wa wakongwe Simba na Yanga kuanzia uwanjani mpaka katika ngazi ya kiuchumi. Mbali ya kuwa wamiliki wa ubingwa wa ligi kuu, Azam ndiyo timu yenye miundo mbinu ya kisasa ambayo Simba n Yanga zitaishia kuiota tu. 

Joseph Marius Omog ana kibarua sasa cha kuiweka Azam FC katika ramani ya afrika.Ana kazi kubwa ya kuweza kumfanya Bakhressa sasa akae meza moja na Moise Katumbi kutembea kifua mbele kwa kuifanya Azam FC iwe klabu kubwa Afrika kama ilivyo Tp Mazembe.

Kushinda tena ligi kuu hakika itakuwa sio mafanikio ya kushangaza kwa kuwa amesajili wachezaji wenye uwezo mkubwa toka kila pembe ya Afrika kwa gharama kubwa. 

Kuelekea msimu mpya wamenunua wachezaji kama Joseph Paterson na Leon Saint-Preux toka Haiti, Mrundi Didier Kavumbagu na Frank Domayo toka Yanga SC ambao wataungana na mastaa bora kabisa walioipatia ubingwa msimu uliopita kama Kipre Tcheche, Michael Balou, John Boko, Agrey Moriss, Abubakary Salum Sure Boy, Mcha Hamis na wengineo.

Kwa ukubwa na ubora kikosi hiki hana kisingizio cha kutoweza kuivusha Azam Fc nje ya mipaka ya Tanzania.. Rekodi Omog kama kocha haitii shaka na Azam hawakufanya makosa walipoamua kumkabidhi timu.
Omog nafikiri ni baada ya kuweza kuiongoza AC leopard kuvunja ukame wao wa miaka 30 bila taji lolote kwa kutwaa kombe la ligi ya kongo mara mbili 2012 na2013 kabla ya kuwapa ubingwa wa kombe la shirikisho kwa kuifunga Djoiba AC ya Mali pia mwaka 2012.

Anajulikana kwa uzoefu wake wa kuweza kuwafanya wachezaji waweze kushindana katika ngazi za kimataifa na kushinda makombe. Msimu wake wa kwanza kuiongoza Azam kushiriki mashindano ya kombe la shirikisho ambayo ana historia ya kushinda haukuwa mzuri sana.Aliondolewa mapema na Ferraviaro ya Beira Msumbiji katika hatua za mwanzo.

Kwa mara ya kwanza sasa anaingia katika historia ya kuiongoza Azam Fc kushindana katika mchuano wa vilabu bingwa bara la Afrika akiwa kama bingwa toka Tanzania bara. Tunaweza kusema kusema uzoefu wa wachezaji na muda mfupi aliokaa nao kuwa ni kigezo cha wao kutokufanya vizuri msimu uliopita.

Msimu huu hawana kisingizio kocha Omog amepata wasaa mzuri wa kukaa na timu muda mrefu na kuwajua vizuri wachezaji wake pia amepata fursa ya kuziba nyufa mahali alipolazimika kufanya hivyo  katika kikosi chake. Ana wajibu wa kuvunja rekodi ya Yanga na Simba kufika hatua ya makundi katika mshindano hayo. 


Akifanya kazi katika timu ambayo haina migogoro ya nje ya uwanja na makundi yanyoweza kuleta mgawanyiko katika timu, Omog atapata muda mzuri wa kuweza kuifanya kazi yake kwa umakini bila shinikizo.

Wamiliki wa Azam wanatakiwa sasa kuona matunda ya uwekezaji wao mkubwa nje ya Tanzania, kama wafanyabiashara ndoto yao ya kuona brand ya Azam Fc ikiwakilisha vizuri kimataifa ni jambo amabalo wamelipigania muda mrefu sana na sasa Omog amebeba matumaini yao hana budi kutimiza ndoto kwa kuwa amepewa vitendea kazi vyote. 

 Haitakuwa tatizo kwa washabiki wa Azam fc kusherehekea mafaniko ya kutwaa taji la ligi kuu bara endapo watatwaa kwa mara ya pili ila ni wakati muafaka sasa waweke mipango  mikubwa ya kushinda vikombe vya kimataifa zaidi ya ligi kuu Tanzania bara na kombe la Mapinduzi. Muda wa kuacha alama yao katika soka la Afrika ni huu.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!