Takribani wiki tatu baada ya kupewa mkataba wa mwaka mmoja kocha wa Simba raia wa Coratia Logarusic ametimuliwa kazi na klabu ya Simba, unaweza kuona ni kitu cha kawaida ila unashtuka kusikia hili hasa kwasababu ni juzi tu klabu ya Simba imepata uongozi mpya chini ya Raisi Evance Aveva.
Uongozi ambao nilitegemea waingie madarakani wakiwa na mawazo tofauti na uongozi uliopita ili kuijenga Simba mpya na yenye mafanikio lakini kumbe ni tofauti na ninachokiona. Nilitarajia kuona uongozi mpya ukija na mikakati mipya kuifanya Simba irejee katika makali yake.
Mikakati ya kuhakikisha uwanja wa Bunju unakamilika, mikakati ya kuhakikisha Simba inarejea kwenye michuano ya kimataifa na zaidi kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara lakini kumbe uongozi ulikuwa na mawazo mfu ya kumpa kocha mkataba wa mwaka mmoja kumbe walimaanisha mkataba wa wiki tatu.
Sikatai kocha Logarusic alikuwa na mapungufu yake na ndiyo maana msimu wa 2013/2014 timu ya Simba haikuwa bora na kupelekea kumaliza ligi kuu nje ya nafasi 3 za juu, lakini kama Logarusic alionekana mbovu kwa msimu uliopita vipi alipewa mkataba mrefu zaidi kuliko ule wa mwaka jana? Hapa ndipo unapopata wasiwasi na maamuzi ya uongozi wa timu ya Simba chini ya Raisi mpya.
Naamini kabisa baada ya kupewa mkataba wa mwaka mmoja Logarusic alianza kuandaa mipango na mikakati ya msimu mpya wa ligi lakini bila kutegemea baada ya kufungwa goli 3-0 na Zesco ya Zambia kwenye mechi ya bonanza siku ya “SIMBA DAY” mkataba wake ukasitishwa na Logarusic akatimuliwa kazi, unawaza uongozi wa Simba walitumia kigezo gani kusitisha mkataba wa Loga?
Kama kocha anaweza kufukuzwa ndani ya wiki tatu baada ya kupewa mkataba wa mwaka mmoja tena baada ya kufungwa kwenye mechi ya bonazan, unatarajia nini kwa kocha mpya atakayekuta tayari wachezaji wapya wameshasailiwa na mtu mwingine? Utaanzia wapi kumlaumu kocha huyo asipofanya vizuri?
Lakini kwa upande wa pili unaweza usishangae sana kwasababu timu kongwe za Simba na Yanga mara nyingi zimekosa uvumilivu dhidi ya makocha wenyeji na hata wageni.
kila uongozi unapoingia madarakani unaingia na siasa zake na kutaka kuleta mafanikio ya haraka ili kuwafurahisha mashabiki bila kuangalia mipango na mikakati ya kocha lakini pia bila kuangalia mahitaji ya timu. Kwa mwendo huu, timu zetu zitafikia kweli mafanikio ya TP Mazembe?
NAWASILISHA
0 comments:
Post a Comment