Searching...
Image and video hosting by TinyPic
13 August 2014
Wednesday, August 13, 2014

Makocha wazawa mko wapi?



Na Abou Hozza

Ni kitambo kidogo toka kocha mzawa aongoze timu ya taifa au klabu na kupata mafanikio. Tangia zama za king Abdallah Mputa Kibadeni aliyeiongoza Simba kufika fainali za kombe la washindi Afrika mwaka 1993 na Tito Mwaluvanda(marehemu) aliyeifikisha Yanga hatua ya nane bora ya mashindano ya timu bingwa za Afrika mwaka 1999, hakuna mwingine mwenye mafanikio ya kujivunia.

Dalili za kuisha kwa ukame wa mafanikio kwa makocha wazawa hazionekani. Timu zote kubwa zenye uhakika wa kuwakilisha nchi kimataifa bado zinaongozwa na makocha wageni. Simba, Yanga na Azam zote zimechagua kutowaamini makocha wa kibongo.

Juma Mwambusi akiwa na Mbeya City kidogo alijaribu kuonyesha kuwa uwezo wa makocha wazawa bado upo. Kama timu kubwa zikiwaamini makocha wa Kitanzania mara nyingi huwa ni kwa ajili ya kuzugia tu huku yuma ya pazia huwa wanawaita ni wasimamizi wa mazoezi. 

Hawaaminiki kama wana mbinu za kuleta ushindi na mfano mzuri ni namna klabu ya Simba inavyowatumia King Kibaden na Jamhuri Kiwhelo.

Leo hawapo kesho watarudishwa tena na keshokutwa watafukuzwa. Wameridhika Simba ipo damuni mwao utawaambia nini. Wanapokuja wageni kufundisha timu zetu, wenyeji wanabakia kuwa makocha wasaidizi au kuwa makocha wa makipa.

Na kibaya zaidi makocha wetu wenyeji pia hawapati hata muda wa kujifunza toka kwa hao wazungu, wakiondoka ni ngumu sana angalau kukabidhiwa jukumu hata kwa muda mfupi. 

Najiuliza hivi toka Kali Ongala aanze kuwa msaidizi wa makocha wa kigeni pale Azam Fc hajapata uzoefu wa kutoka na kufundisha klabu nyingine akiwa kocha mkuu? 

Ni kama ilivyo kwa Seleman Matola ameweza kuingoza timu ya Simba ya vijana kuweza kufanya vizuri kwa muda mrefu sana katika soka la vijana. 

Pia ametumika kama kocha msaidizi kwa nyakati tofauti mpaka sasa bado Simba hawajamwamini na kumkabidhi timu.

Matola anaweza kuwa ana mchango mkubwa sana ndani ya Simba kuliko makocha wote wageni wa hivi karibuni wengi wamekuja na kukuta msingi wa wachezaji vijana waliopikwa vizuri chini ya Matola. 

Matola ndio mpishi wa kizazi kipya cha Simba chenye vijana wenye uwezo mkubwa,  ndiye aliyewafanya watu kama Christopher Edward, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, William Lucian, Said Ndemla na vijana wengine leo hii wawe wachezaji wakubwa.

Kama aliweza kuzalisha kizazi hiki cha kuvutia, kwa nini Simba wasimuamini na kumpa timu ya wakubwa? Sijajua kama Matola ana mpango wa kuwa msaidizi mpaka lini lakini, kama Simba wanashindwa kumuamini na yeye anasubiri nini kwenda hatua moja mbele?

Hata timu yetu ya taifa sasa imegeuka kuwa maskani ya makocha wa kigeni. Silvester Marsh ametumika timu ya taifa karibia chini ya makocha wote wazungu kuanzia kipindi cha Maximo. 

Ameiongoza timu ya taifa ya vijana mara kadhaa lakini  bado ana kibarua cha ukocha msaidizi labda leseni yake ya ukocha haimhuruhusu kuwa kocha mkuu ama la TFF inashindwa kumuamini?.

Lazima sasa atuonyeshe kwa vitendo alichojifunza toka kwa makocha wa kigeni. Ninavyofahamu mimi ni kwamba kuwa kocha msaidizi sio kwamba umeandikiwa hivyo milele ni fursa ya kufanya kazi chini ya mtu aliyekuzidi vigezo na kupata uzoefu kupitia kwake.

Jose Mourinho ametokea katika mikono ya Bob Robson na leo ni kocha mkubwa duniani, Ryan Giggs yupo shule akijifunza kupitia kwa Luis Van Gaal, ndoto yake ni kuingoza United siku moja. Tunahitaji na sisi kubadilika na kupita njia hizi hizi.

Tunahitaji sana kizazi kipya cha makocha wa kitanzania katika mpira wetu, hivyo makocha wetu wanapaswa sasa kujiamini na kuchangamkia fursa. 

Wajitahidi kuwa wezi wa ujuzi wapatapo nafasi ya kufanya kazi na wageni na sio kuridhika kuwa wasaidizi milele daima. 

Wazidi kuitafuta elimu mpya ya mpira ili waweze kuendana na ubora wa mpira ambao kila siku unazidi kuwa unachezwa kisasa.Ni aibu kuzidi kuwaacha wageni kutawala katika soka letu. 

Na muhimu pia makocha wetu wasiishie hapa tu wavuke mipaka na kwenda hata kufundisha nchi za jirani.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!