Na Mwandishi wetu
Nilimuona Ramadhani Singano Messi akiwa bado mchanga zaidi ya sasa, nikamuona Edward Christopher akiwa kinda na Jonas mkude wakiwa kwenye fomu kama wamecheza misimu zaidi ya kumi ya ligi kuu.
Simba ikawa inajivunia matunda yao ya timu ya vijana na hakika ilimeremeta na hakuna ubishi walikuwa wameanza kushika kasi yao ambayo ilikuwa hauwezi kuizima kwa kirahisi sana.
Lakini mafanikio haya yote yalikuja nyuma ya benchi la ufundi imara lililokuwa chini ya mserbia Prof Milovan Cirkovic.
Hakika Simba ilitakata sana na ikafikia hatua mtani akala tano bila mbele ya mashabiki 60,000 pale Uwanja wa taifa. Milovan alikuja na falsafa nzuri ya kuijenga simba yenye kucheza soka la kipekee kupitia msingi wa timu ya vijana “Simba B”.
Na kwa hilo alifanikiwa maana yeye pekee ndio alikuwa na uthubutu wa kuwapanga chipukizi hao tena kwenye mechi kubwa na wakapata matokeo mazuri.
Makocha wengi wa timu hizi kubwa walikuwa wanaogopa kuwatumia chipukizi kwa kuhofia kutimuliwa pindi timu itakapopata matokeo mabovu.
Tamthilia ya viongozi kuwapangia makocha wachezaji wa kucheza ilikuwa imetawala katika klabu hizi kongwe nchini lakini Milovan alipambana nazo kwa hali na mali.
Naikumbuka mechi ya mwisho ambayo ilikatiza safari ya Milovan ilikuwa kati ya Simba na Mtibwa pale Morogoro.
Bada ya mechi ile viongozi ambao daima huwa wanakimbilia kufukuza makocha haswa timu ikipata matoke mabovu walimtupia mzigo wa lawama mzungu wa watu kitu ambacho niliamini hakuwa na hatia.
Ni kweli Simba ilicheza mechi takribani tano za ugenini na haikupata matokeo mazuri, lakini matokeo yale hayakuwa na mahusiano yeyote na kocha kwa maana timu inakosa pointi tatu lakini kazi inafanyika.
Mpira unapigwa sawa sawa na unaona kikosi kikicheza kitimu lakini kama ilivyo mchezo wa soka una matokeo matatu mwisho wa siku wanakosa kupata matokeo mazuri.
Baada ya hapo kocha ambaye binafsi naamini ni kocha bora kwa Simba katika kipindi cha miaka kumi akafungashiwa virago.
Nilisikitika sana kwa maana nikiwa kama mpenda soka nilijua kuwa Simba haikumtendea haki Milovan, Kocha ambaye alitumia muda wake wote na nguvu zake zote kuhakikisha anajengea timu bora ya miaka yote.
Baada ya hapo nikaanza kuona maigizo ya kuleta makocha mbalimbali lakini moyoni mwangu nilijua na ninajua kuwa hakuna wa kuweza kuvaa viatu vya Milovan.
simba haikupaswa kurudi nyuma Mwandishi mashughuli wa vitabu duniani Nappoleon Hill katika kitabu chake cha “THINK AND GROW RIC” aliandika kuwa siku zote ukitaka kuanzisha jambo basi wapaswa kuanzia maeneo ya karibu na alipoishia mwenzako hivyo usiende mbali sana zaidi ya alipoishia mwenzako.
Simba walipaswa kutafuta Mwalimu mwenye uwezo zaidi ya Milovan, mwenye kujua thamani ya kujenga timu bora ya muda wote na sio vikosi zimamoto.
Katika hili hawakufanikiwa hata kidogo maana waliokuja baada ya Milovan walikuwa ni aibu na uozo, Kuanzia Leiewing hadi Lagarusic.
Kwa upande wangu kidogo Kibadeni alijaribu kuvaa lakini naye yeye aliponzwa na dhana ya kuwa makocha wazawa sio bora zaidi ya hawa wenzetu weupe.
Nilitambua mchezo wa soka ni mchezo wa makosa hivyo hata viongozi walikuwa wamekosea kumfukuza Milovan.
Walimfukuza kwa masimango na lawama kibao za kusingizia. Uongozi ulikuwa unaficha maovu yao kupitia kocha na binafsi nilikiri kuwa Masikitiko ya Milovan yataitesa sana Simba Sports Club.
Jana wamemtimua Loga, nadhani viongozi wanatambua wajibu wao. Nawapa ushauri wamrudishe kundini Milovan arudishe ladha ya mpira Msimbazi.
0 comments:
Post a Comment