NIONAVYO MIMI:BUSARA ZA MANUEL PELLEGRINI ZIMENIPA SOMO.
Na Oscar Oscar Jr
+255789784858
Ilikuwa ni jambo la kawaida sana kwenye miaka ya 1990 kuona watu wakisimama kwa muda pale bendera ya taifa inapokuwa ama inapandishwa au kushushwa.Ilikuwa ni fahari kusimama pindi unaposikia wimbo wa taifa ukiimbwa,kwa sasa jambo hilo halipo na kama lipo ni kwa kiasi kidogo sana.Ni jambo la kawaida tu siku hizi kuona mtu akitembea huku akitafuna muhindi wa kuchoma wakati wimbo wa taifa ukiimbwa!
Ni lazima tuondoe chuki katika maisha na tujivike busara,uzalendo na kuonyesha wazi hisia zetu pale tunapopata nafasi ya kufanya hivyo.Kocha wa Manchester City,Manuel Pellegrini hakutaka kuwa mnafiki pamoja nakuwa timu yake ilipoteza mchezo wao dhidi ya Liverpool,bado hakuona kama ni busara kwa mtu kama yeye kuondoka uwanjani bila kushikana mkono na kaka mkubwa,Steven Gerrard.
Baada ya mechi kumalizika na Liverpool kuibuka na ushindi wa bao 3-2,Gerrard alitawaliwa na furaha ya hali ya juu na alibaki uwanjani akishangilia huku machozi yakimtoka kwa muda mrefu lakini,Manuel Pellegrini aliendele kumsubiri na mwishowe alifanikiwa kumshika mkono na kumpa pongezi.Asante Pellegrini kwa kuonyesha heshima dhidi ya Steven Gerrard.
Manchester City ni klabu ambayo tulizoea kusikia kila siku vurugu,leo ukisikia Carlos Tevez amekunjana mashati na kocha Roberto Mancini,kesho yake utasikia,Super Mario Balotelli amezichapa na kocha wake mazoezini.Pamoja na kutomudu wachezaji wake,ni lazima pia nimpe heshima Manchini kwa kuwapatia kombe la FA na lile la EPL ambalo walilisubiri kwa muda wa miaka 44.Vurugu kama hizo kwenye utawala wa Pellegrini hazipo tena.
Pellegrini ni kocha mwenye busara sana,si mtu mwenye papara bila kujali kama ameshinda au amepoteza mchezo.Manchester City chini ya Pellegrini wamekuwa wazuri sana wanapocheza uwanja wa nyumbani pale Etihad lakini,wamekuwa sio wazuri sana wanapokuwa ugenini.Moja ya vichapo vyao vya ugenini ambavyo pengine havikutarajiwa,ni kile walichopewa na Sunderland pale Stadium Of Light na kule Wales dhidi ya Carddiff City lakini,bado Pellegrini aliendelea kuwa mtulivu.
Man City wanatembeza bakora sana wanapokuwa dimba la nyumbani,Arsenal alichezea 6-3,Norwich City 7-0,Spurs 6-0 na mahasimu wao,Man United walichezea 4-1 lakini,Pellegrini aliendelea kufanya kazi yake kwa utulivu na ustadi wa hali ya juu sana na ni Chelsea tu ambao walifanikiwa kuchomoza na ushindi kwenye dimba hilo la Etihad.Kwa kifupi unaweza kusema,Pellegrini ameufanya uwanja wa Etihad ufanane na viwanja vya mchezo wa Tenisi ambavyo siku zote matokeo yake hutolewa kwa mfumo wa seti.
Heshima ni kitu cha bure hata kama umri wako ni mdogo lakini kama utakuwa unajiheshimu na kufanya kazi yako vema,kila mtu atakupenda.Wakati wewe hutaki kwa chuki zako binafsi kusimama hata kwa sekunde kadhaa kuipongeza timu ya Azam kwa kuwa mabingwa wapya wa ligi kuu Tanzania bara,Pellegrini alibaki kasimama akimsubiri Steven Gerrard ambaye hakuwa hata na habari kama anasubiriwa!
Gerrard ni moja kati ya wachezaji wachache waliobaki ambao heshima na nidhamu yao ya mchezo wa soka,siku zote itabaki katika vitabu vya kumbukumbu barani Ulaya na Dunia kwa ujumla.Pellegrini hakupoteza muda bure,kuna jambo analiona ndani ya kiungo Steven Gerrard.Kuna muda unaona kabisa kuwa mpira hautendi haki,mtu kama Tom Clevery (Sina nia ya kumdharau) ameshinda medali ya ligi kuu akiwa na Manchester United lakini,kaka mkubwa Gerrard,hana kitu! unadhani mpira umetenda haki hapa? hapana,Gerrard anastahili medali hii.
Mchezo wa soka uzuri wake ni kwamba,unachezwa sehemu ya wazi,kila mtu anauona.Ni vema tukajifunza kukubali kushindwa na kuacha chuki zisizo na msingi na pia,kuonyesha heshima kwa mtu unayemkubali akiwa hai ina leta maana zaidi.Kwani ukisema Amisi Tambwe ni balaa,kuna mtu atapinga? akijitokeza mtu mbishi,mtolee orodha ya wafungaji bora wa ligi kuu Tanzania bara msimu huu.Ukiona anaendelea kukubishia,mlete kwangu.
Nadhani kuna kitu bado hatukijui,kumpa sifa na heshima mtu unayempenda tena akiwa hai,inamaana kubwa sana kuliko kumwagia sifa pale ambapo ametangulia mbele za haki.Mrisho Ngassa,Mwagane Yeya na Amisi Tambwe,hawa ndiyo mashujaa wangu wa ligi kuu msimu huu ambao unaelekea ukingoni na nikipata nafasi,nitasimama kama Pellegrini alivyofanya na kuwashika mkono.Unataka kuniuliza swali? hapana,ngoja mimi ndo nikuanze,unajua kama hawa ndiyo wazee wa Hat-trick msimu huu? Kipre Tchetche anamagoli 13 na kaipa Azam Ubingwa,nikimsifia ni dhambi? acheni nongwa bwana!
Naomba nisimame kwa muda na kuwashika mkono Azam Media Group.Nataka nionyesha busara kama za Pellegrini kwenu katika mambo makubwa mawili.Kwanza ni ubingwa na pili,ni kufanikisha kwenu kutuletea michuano ya ligi kuu bara moja kwa moja.Mmewafanya viongozi wa timu za Kariakoo wakose cha kutudanganya pindi walipoangukia pua huko mikoani,wamebaki wanazusha leo rushwa,na kesho uchawi ambao hawawezi hata kuuthibitisha.Kama wao tu Simba na Yanga wameshindwa kuifunga Azam,iweje watake timu nyingine ndiyo zimfunge? jamani,njooni tu muungane na mimi kisha tufanye kama Pelllegini na Gerrard.Mchezo umekwisha,tukutane msimu ujao.
Pamoja na kuwa Pellegrini amefanikiwa kutwaa taji la Capital one msimu huu lakini ukitazama ukubwa na ubora wa kikosi chake,utakubaliana na mimi kuwa taji hilo moja halitoshi.Wakati Man City wanakula kichapo mechi yao ya kwanza dhidi ya Barcelona kwenye hatua ya mtoano klabu bingwa Ulaya,Pellegrini alitaka kuhamaki na kutoa shutuma nyingi kwa mwamuzi wa mchezo ule.Baadae,aligundua kuwa alifanya makosa na akakubali kurudi na kuomba msamaha kutokana na kauli yake.Ni nani asiyekosea? jibu ni hakuna lakini, ni wangapi wenye busara za kuomba msamaha pindi wanapokosea? usinipe jibu.
Soka ni mchezo wa watu wastaarabu,watu wanaokubali kushindwa,watu wanaokubali kupokea changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.Kama kuna mtu anafanya vizuri iwe ni kwenye Soka,Muziki,Siasa au kitu chochote,usisubiri mpaka afe ndiyo aunze kumwagia sifa.Utapungukiwa nini ukinisubiri ili unishike mkono kwa dakika japo tano tu? usijifiche mtu wangu popote utakapo niona,nisubiri japo unishike mkono.Heshima kwako kaka mkubwa Gerrard,heshima kwako mzee wa busara Manuel Pellegrini,nawatakia wote kila la kheri kwenye mbio hizo za EPL.
Kwa leo,naishia hapa.Naomba kutoa hoja na kama unachochote ambacho ungependa kunishirikisha,nitafute kwenye ukurasa wangu wa Facebook au unaweza kuchati na mimi kwenye whatssap kwenye namba +255789784858
0 comments:
Post a Comment