Searching...
Image and video hosting by TinyPic
13 April 2014
Sunday, April 13, 2014

LIVERPOOOL WAITWANGA MAN CITY 3-2 PALE ANFIELD



Na Oscar Oscar Jr
+255789784858
Viongozi wa Ligi ya Premia Liverpool walipiga hatua kubwa katika safari yao ya kutaka kuwa mabingwa wa Uingereza kwa mara ya kwanza katika miaka 24 walipowatwanga Manchester City walio nambari tatu 3-2 katika uwanja wa Anfield Jumapili, ukiwa ndio ushindi wao wa 10 mfululizo. 

Klabu hiyo ya Merseyside haijashinda taji tangu 1990, miaka miwili kabla ya enzi ya Ligi ya Premia kuanza.
Raheem Sterling na Martin Skrtel waliwaweka 2-0 mbele katika dakika 26 kabla ya David Silva kuongoza ufufuo wa City. Mhispania huyo alichomoa bao moja, naye Glen Johnson akajifunga dakika tano baadaye na timu zikawa zimetoshana nguvu. 

Lakini Mbrazil Philippe Coutinho alifunga bao la ushindi baada ya kosa la nahodha wa City Vincent Kompany.
Jordan Henderson wa Liverpool alifukuzwa uwanjani kwa kupewa kadi nyekundu muda wa ziada na atakosa mechi tatu kati ya mechi nne zilizosalia. 

Liverpool sasa wako alama saba mbele ya City, baada ya kucheza mechi mbili zaidi, na wako alama tano mbele ya wageni wao wajao Chelsea, ambao walikuwa wacheze dhidi ya Swansea baadaye Jumapili. 

Ilikuwa siku ya hisia nyingi kwa klabu hiyo, iliyokuwa pia ikiadhimisha miaka 25 tangu kutokea kwa mkasa wa Hillsborough uliopelekea vifo vya mashabiki 96 wa klabu hiyo wakati wa nusufainali ya Kombe la FA. 

Kulikuwa na dakika moja ya kimya kabla ya mechi kuanza, na baadae mashabiki walishabikia timu yao na bao la kwanza likapatikana dakika ya sita. 

Luis Suarez alimzidi nguvu Gael Clichy na kusambaza mpira kwa Sterling, na tineja huyo kwa ustadi akamchenga Kompany na kisha kipa wa Uingereza Joe Hart kabla ya kufunga. 

Dakika ishirini baadaye, Hart aliokoa vyema mpira wa kichwa kutoka kwa nahodha wa Liverpool Steven Gerrard aliyekuwa hana wa kumkaba, lakini akatoa mpira na ukawa kona ambayo difenda wa Slovakia Skrtel alifunga.


Hapo katikati, City walipoteza kiungo wao wa kati kutoka Ivory Coast Yaya Toure ambaye amewafaa sana na ilikuwa ni hadi muda mfupi kabla ya muda wa mapumziko ambapo walitishia Liverpool. 

Johnson na Sterling walilazimika kutoa mpira kutoka kwenye mstari kwenye shambulio moja na kombora la Fernandinho likaokolewa na kipa Simon Mignolet. 

City, waliokuwa mabingwa miaka miwili iliyopita kabla ya kupokonywa taji na majirani zao Manchester United msimu uliopita, waliendelea kuimarika baada ya muda wa mapumziko huku James Milner na kisha Sergio Aguero wakiingia uwanjani. 

Dakika ya 56, Milner alimwandalia mpira Silva naye hakusita na akafunga kutoka karibu na goli. Dakika tano baadaye Silva na Samir Nasri walibadilishana pasi safi na matokeo yake ukawa mpira ambao ulipinduliwa na Johnson na kubwaga kipa wake.

Daniel Sturridge wa Liverpool, ambaye aliwahi kuchezea City, na mwenzake Suarez wote walitaka wapewe penalti katika visa tofauti lakini video za marudio za televisheni zilionyesha Suarez alikuwa amepiga mbizi na,ukizingatia kwamba alikuwa tayari ameonyeshwa kadi ya njano awali, alifaa kufukuzwa uwanjani kwa kadi nyekundu. 

City walikuwa wameanza kuonekana kama wangeshinda licha ya mwanzo wao mbaya na Mignolet alilazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia Edin Dzeko asifunge kabla ya Silva naye kushindwa kidogo tu kuifikia krosi murua kutoka kwa Aguero. 

Lakini Liverpool waliamka tena. Kompany aliondoa vibaya mpira na Coutinho akambwaga Hart kwa kombora safi la chini kutoka hatua 15. 

Kadi nyekundu ya Henderson ilitokana na kumwendea Nasri vibaya na kusimamishwa kwake kucheza kutamfanya akose mechi tatu muhimu, ikiwemo moja dhidi ya Chelsea walio nambari mbili ambayo itachezwa wiki mbili zijazo. 

Kipenga cha mwisho kilipopulizwa, Gerrard alikusanya wachezaji wake katikati ya uwanja huku mashabiki wenyeji wakishangilia ajabu. 

Liverpool wanahitajika kuinyuka Chelsea ndipo washinde taji lakini ushindi huu wa kusisimua bila shaka umewaweka katika nafasi bora zaidi.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!