KUELEKEA REAL MADRID VS BORUSSIA DORTMUND.
Real Madrid wanapong’ang’ana kuendeleza juhudi zao za kupigania taji la La Liga, wana azma pia ya kushinda taji lao la 10 Ulaya na wiki hii watakutana na Borussia Dortmund ambao waliwazima msimu uliopita.
Kila mwaka unavyosonga, hamu ya Real kushinda taji la 10 la Ulaya, au ‘decima’, imekuwa ikiongezeka na rais wao Florentino Perez alitumia pesa nyingi sana kujaribu kutimiza hilo kwa kutwaa nyota kutoka kila kona duniani.
Walishinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara ya mwisho 2002 na matumaini yao yaliongezwa mara nyingine tena msimu uliopita walipofika nusufainali lakini wakabanduliwa na Borussia Dortmund ambao hawakuwa wanapigiwa upatu kushinda.
Watakabiliana tena kwenye mechi ya kwanza ya robofainali yao Jumatano huku Real wakiwa na presha ya kufana barani baada ya kutwangwa mara mbili kwenye mechi tatu za ligi na kuteleza kwenye juhudi zao za kupigania taji la nyumbani, baada ya wao kwenda muda mrefu bila kushindwa.
.
Real wanakutana na timu ya Dortmund ambayo imelemazwa na mejaraha msimu wote lakini kocha wao Jurgen Klopp anaamini kwamba wanaweza kushangaza miamba hao tena Bernabeu.
"Ukizingatia bajeti yetu na majeraha…hatupigiwi upatu kushinda,” aliambia gazeti la Uhispania la Marca.
"Hata hivyo, huwa nasema kwamba si lazima kuwa timu bora zaidi duniani ndipo uweze kulaza timu bora zaidi duniani mnapokutana, na Borussia inaweza kuwatwanga walio bora.
“Hili ndilo jambo muhimu zaidi kwangu. Borussia wana nafasi na labda tutawashika.”
Pamoja na wachezaji ambao wanauguza majeraha, pia watakosa straika wao matata Robert Lewandowski, ambaye amesimamishwa kucheza mechi ya kwanza.
“Umekuwa msimu mgumu kuanzia mwanzo. Tumekuwa na changamoto nyingi sana na mzozo wa mejaraha ambao haukutarajiwa,” Klopp akaongeza.
“Sijawahi kuona kingine cha kufananisha na hili lakini licha ya haya yote, tuko kwenye nafasi bora ya kutimiza malengo yote tuliyoweka mwanzoni mwa msimu.
“Tutacheza kama kawaida yetu. Tutajaribu kucheza mchezo wetu bernabeu. Madrid wanapigiwa upatu kushinda lakini tutajaribu na kupata matokeo ambayo yatatupa fursa mechi ya marudiano.”
Real walijibu vichapo hivyo mfululizo, kimoja kikitoka kwa Barcelona, kwa kupata ushindi mkubwa wa 5-0 wikendi dhidi ya Rayo Vallecano.
"Tunakaribia mwisho na huenda ikawa bora baada ya kutwangwa mara mbili lakini tuko katika hali nzuri. Kiakili tulifanya vyena na tuna matumaini,” kocha Carlo Ancelotti aliambia kikao cha wanahabari.
"Jumatano, tutakuwa na mazingira mema (kwenye uwanja). Kila mmoja ana ndoto, ya kombe la kumi, na kila mmoja anaelewa kwamba tunaweza kushinda kama tutasalia tukiwa tumeungana na tunaweza kutimiza ndoto hiyo.”
0 comments:
Post a Comment