KUELEKEA PSG VS CHELSEA HAPO KESHO.
Paris St Germain lazima wasiwe na huruma kwenye goli wakatapokutana na mabingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2012 Chelsea kwenye mechi ya kwanza ya robofainali ya ligi hiyo Jumatano, haya ni kwa mujibu wa kocha wao Laurent Blanc.
Mabingwa hao wateule wa Ligue 1 wameenda mechi nane wakishinda zote katika mashindano yote lakini beki huyo wa kati wa zamani wa Ufaransa anajua kwamba Chelsea, chini ya Jose Mourinho, wana uzoefu na ujuzi wa kujilinda na kuzima wapinzani wowote.
"Lazima tuwe wakali zaidi,” akasema Blanc. “Tutakuwa na nafasi chache sana na tunapozipata lazima tufunge.
“Tunajua kwamba tutahitajika kuwa katika kiwango kingine,” aliongeza kuhusu mechi hiyo itakayochezewa Parc des Princes.
Kikosi ghali sana cha Blanc hakina wa kukizidi katika ligi ya nyumbani, na wako mbele ya Monaco walio nambari mbili kwa alama 13 wakiwa na mechi saba waliosalia nazo msimu huu.
PSG pia walisonga hadi awamu ya muondoano Ligi ya Mabingwa kutoka kwa kundi lililokuwa na Anderlecht, Porto na Olympiacos Piraeus na kisha wakaibandua Bayer Leverkusen kwenye 16 bora.
Mkombozi kwenye mechi zote mbili dhidi ya Chelsea huenda akama straika nyota wa Blanc, Zlatan Ibrahimovic ambaye amekuwa hashikiki.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden ndiye anayeongoza kwa ufungaji wa mabao Ligue 1 akiwa mbele sana ya wapinzani wake akiwa na magoli 25. Ameacha mchezaji mwenzake Edinson Cavani na Alexandre Lacazette wa Olympique Lyon wanaoshikilia nambari mbili kwa pamoja kwa mabao 11.
Ibrahimovic pia ametamba katika Ligi ya Mabingwa, na amefunga mabao 10 msimu huu.
PSG, labda kwa sababu ya kuweka jicho moja kwenye mechi hiyo ya Chelsea, hawakucheza vyema dhidi ya Nice Jumamosi na walihitaji bao la kujifunga kupata ushindi wa 1-0.
Viongozi hao wa Ligue 1 wanatarajiwa kuwa kamili ingawa kuna shaka kuhusu Thiago Silva.
Beki huyo wa kati wa Brazil huenda akacheze akiwa na kifaa cha kujikinga usoni baada ya kujeruhiwa shavu lake siku 11 zilizopita.
Silva na beki wa pembeni Gregory van der Wiel, ambaye anauguza jeraha la goti, walipumzishwa wakati wa mechi ya Nice.
Mara ya mwisho Chelsea walizuru Parc des Princes kwenye awamu ya makundi msimu wa 2004-05, kwa mechi ya kwanza ya Mourinho ulaya akiwa meneja wa klabu hiyo ya London, na wakati huo waliitwanga PSG 3-0.
Mourinho atataka sana matokeo mazuri kutoka kwa wachezaji wao baada yao kulala wakati wa kichapo cha 1-0 Jumamosi wakiwa kwa timu inayohangaika kwenye ligi ya Crystal Palace.
Chelsea walijikokota safu ya kati na walikuwa butu safu ya mashambulizi, na kufanya Mreno huyo kusema kwamba ndoto ya kushinda Ligi ya Premia sasa imetibuka.
Kiungo wa kati Nemanja Matic na winga Mohamed Salah hawaruhusiwi kucheza, baada yao kujiunga na Chelsea wakati wa kipindi cha kuhama wachezaji Januari.
Kiungo muhimu wa Brazil Willian anafaa kurudi baada ya kupumzishwa Palace huku Mourinho akitarajia kwamba Samuel Eto'o anaweza kurudi kwenye safu ya mashambulizi baada ya kupata jeraha la misuli ya paja dhidi ya Arsenal wikendi mbili zilizopita.
0 comments:
Post a Comment