YAYA TOURE APIGA HAT-TRICK MAN CITY VS FULHAM
Kiungo machachari wa Ivory Coast, Yaya Toure, alitamba kwa kishindo na kusaidia klabu yake ya Manchester City kuendelea kushamiri katika ligi ya Premier ya Uingereza pale alipofunga mabao matatu katika ushindi wao wa 5-0 dhidi ya Fulham nyumbani kwao Etihad.
Fulham, ambao wanashikilia mkia katika shindano hilo, walichangia kuchakazwa kwao pale mlinda ngome wao, Fernando Amorebieta, aliposababisha penalti mbili na kupokea kadi nyekundu kwa kucheza visivyo eneo la hatari.
Toure alipachika mikwaju hiyo ya adhabu wavuni kuwapa City uongozi wa 2-0 katika dakika za 25 na 52 huku akimzidia kipa wa Fulham David Stockdale aliyeruka upande kinyume na mpira mtawalia.
Amorebieta alitimuliwa kiwanjani baada ya kukosa kupata kadi ya njano katika kisa cha kwanza pala alipompiga mshambuliaji wa Hispania, Alvaro Negredo, teke la nyuma katika kipindi cha kwanza lakini refa Jonathan Moss hakumsamehe kipindi cha lala salama pale alipomfyeka kiungo David Silva, pia wa Hispania katika eneo la hatari.
Huku wakicheza dhidi ya watu 10, City walivizia lango la wapinzani wao na Toure alifanikiwa kukamilisha ‘hat-trick’ yake pale alipofungua shuti nzito kutoka mkwaju wa adhabu hatua 25 kutoka lango pale alipotanguliziwa mpira na Mfaransa Samir Nasri.
Kiungo wa Brazil, Fernandinho aliongeza la nne ikisalia dakika sita mechi kukatika kabla ya mlinda ngome wa Argentina, Martin Demichelis, kukamilisha kichapo hicho katika dakika ya 88 pale Stockdale alipodundisha kombora la Stevan Jovetic hadi guu lake.
0 comments:
Post a Comment