NIONAVYO MIMI:MAN UNITED INAMUHITAJI MWANAMKE.
Na Oscar Oscar Jr
+255789-784858
Kila mwanadamu ameumbwa kwa namna yake na mwenyezi Mungu amemjaalia uwezo wa kufanya jambo ambalo pengine,hakuna mwingine anayeweza kufanya.Wanawake ni viumbe ambao mimi nawaheshimu sana na katika hili,huwa nawapigia "salute" kwa uwezo wao wa kuzaa waliobarikiwa na Mwenyezi na pili,ni uwezo wao wa "kidaktari" ambao hata hawakuusomea.
Daktari aliyesoma Muhimbili kwa miaka 5,anategemea zaidi maelezo ya mgonjwa ili kuweza kubaini tatizo lakini,mwanamke ambaye pengine hakwenda hata darasa moja,anauwezo wa kujua tatizo la mtoto hata wa miezi miwili ambaye haongei wala kutembea,hongereni kina mama.Kumtibu mtoto asiyeweza kujieleza ni kazi sana ambayo naifananisha na ile ya kugundua tatizo la klabu ya Manchester United chini ya kocha mpya,David Moyes.
Nimetumia muda wangu mwingi sana kusoma makala za kaka yangu Israel Saria,Edo Kumwembe na kugundua kuwa kila mtu anabainisha sababu tofauti za kuporomoka kwa Man United.Nimemsikiliza sana Shaffih Dauda na Ibrahim Masoud,nao kila mtu anasababu zake ambazo hazifanani na mwenzie.Nawashukuru sana,angalau nimepata pa kuanzia.
Nikaamua kubadilisha "Chaneli" na kumsoma mchambuzi wa gazeti la "The Telegraph" Alan Hansen,naye nikakuta ameorodhesha sababu zake nyingi sana ambazo ziko tofauti.Nikaona ngoja niende Nigeria kumtafuta mchezaji wa zamani na mchambuzi kwa sasa wa soka,Sunday Oliseh,nilichokikuta huko,pia ni tofauti na hawa wote niliowataja!
Kuna kitu nimegundua,ukiona kila mchambuzi anakuja na sababu zake ambazo hazifanani na mtu yoyote au zikafanana moja au mbili,ni lazima ujue kuwa,tatizo hilo linamuhitaji "Mwanamke" anayeweza kugundua ugonjwa hata wa mtoto wa wiki 3 ambaye hajui kutofautisha kati ya ziwa la mama na lile la ng"ombe.Haiwezekani daktari wa Muhimbili aseme kuwa tatizo ni Malaria,daktari wa Afrika ya Kusini,aseme ni Taifodi,na yule wa India,aseme tatizo ni Uti wa mgongo kwa mgonjwa yule yule,haiwezekani!
Kuna klabu nyingi kwa sasa duniani ambazo ukubwa wa jina la timu,hauendani na kiwango wanachokionyesha uwanjani.Timu za Inter Millan na Ac Millan kutoka Italia ni miongoni na katika zoezi hilo,huwezi kuacha kutaja jina la Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Uingereza,klabu ya Manchester United.
Kocha David Moyes alipewa jukumu la kuinoa Man United msimu huu huku,akipewa mkataba mnono wa miaka 6.Unajua kwa nini alipewa mkataba mrefu kiasi hicho? jibu ni rahisi tu,Kwenda kukaa kwenye kiti alichoacha kocha Sir Alex Ferguson huku akiwa ameshinda mataji 13 ya EPL,makombe 5 ya FA,makombe 2 ya klabu bingwa Ulaya na mengine lukuki,sio kitu cha mchezo.Hakuna kocha kwa sasa Duniani anayeweza kuziba kabisa pengo la Sir Alex Ferguson ingawa,wapo wanaoweza kufanya vizuri na United.
Baada ya Man United kufungwa mchezo wa kwanza wa klabu bingwa ulaya dhidi ya Olympiacos kwa mabao 2-0 kule Ugiriki na kuja kuchezea kichapo cha 3-0 kutoka kwa mahasimu wao klabu ya Liverpool,watu wengi waligeuka kuwa "wanawake" na kuanza kueleza matatizo ya United na wengine,walikwenda mbali zaidi na kutaka Uongozi wa Man United,umtimue kazi kocha huyo!
Magazeti mbalimbali ya Uingereza yamejaribu kubainisha sababu za kutaka kocha David Moyes atimuliwe,chache kati ya hizo ni kukosa uzoefu,kushindwa kuwamudu wachezaji wakubwa,mbinu mbovu,kushindwa kuongea vizuri na vyombo vya habari na nyingine kibao.Ukichunguza sababu hizo,utagundua kuwa,zipo zenye mashiko na nyingine ni "Upupu mtupu".
Wakati makocha wenye uzoefu wa kuongoza klabu kubwa duniani na wachezaji wenye majina makubwa kama kocha Arsene Wenger na Manuel Pellegrin wakifungasha virago mapema kwenye ligi ya Mabingwa,kocha asiye na Uzoefu,asiyejua kuongea na vyombo vya habari David Moyes,kabaki na kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
Sir Alex Ferguson tangu afike fainali ya klabu bingwa na kutetemeshwa na Barcelona pale Wembley msimu wa 2010/2011,hajawaki kufika tena hata kwenye hii robo fainali aliyofika msimu huu kocha David Moyes.Msimu wa 2011/2012,United chini ya Ferguson walitolewa kwenye hatua ya makundi tu na kwenda Europa League ambako nako,walitia aibu tu.Msimu wa 2012/2013,United walitolewa tena kwenye hatua ya mtoano dhidi ya klabu ya Real Madrid.
Kuna muda watu wanaandaa majibu,kabla hata ya kujua maswali yataulizwaje! watu wengi waliamini kuja kwa Moyes,Rooney hawezi kubaki Old Trafford lakini,Moyes amefanikiwa kumtuliza "baba wa united" Wazza lakini,watu hawaoni pia kama hiyo ni faida kwa timu.Moyes ni kocha wa kiwango cha kati sawa tu na kocha wa Liverpool Brendan Rogers,anahitaji muda na kuungwa mkono.Brendan Rogers anazidiwa ukubwa na klabu ya Liverpool lakini,kwa sababu ameaminiwa na kupewa muda huku akiungwa mkono,amefanikiwa sasa kuibadilisha Liverpool.
Wakati msimu ukiendelea,Moyes ameonekana viwanja mbalimbali akiangalia wachezaji ambao anaweza kufanyanao kazi.Kuna muda alionekana Signal Iduna Park,nyumbani kwa Borussia Dortmund na ilisemekana lengo ni kumtazama kiungo,Ilkay Gundogan na Marco Reus.Kuna muda alionekana Stadio Olympico nyumbani kwa Juventus,akimtazama Arturo Vidal na Paul Pogba na kama hiyo haitoshi,alikwenda mpaka Estadio Vincent Carderon nyumbani kwa Atletico Madrid kumtazama kiungo Koke na mshambuliaji Diego Costa.Ziara kama hizi sio za mpango wa muda mfupi,David Moyes ni lazima abaki United na msimu ujao,timu itazaliwa upya.
Tatizo mgonjwa akishaugua kwa muda mrefu,huwa hachagui pa kwenda.Ukimwambia kuna sangoma anatibu yuko Tanga,atakwenda.Ukimwambia kuna mchungaji anaombea watu yuko Tabora,nako atakwenda.Ukimwambia kuna mtu anatibu kwa kutumia Computer,nako atataka kwenda! basi tabu tupu!
Kagawa alinunuliwa kama mbadala wa Wayne Rooney ambaye kocha Sir Alex Ferguson alikuwa na mpango wa kumpiga bei,ujio wa Moyes,Rooney kakubali kubaki na Moyes kaonyesha kumuhitaji,Kagawa hana chake tena.Hawezi kucheza kwa mafanikio namba nyingine tofauti na namba 10,mara kadhaa amepelekwa nafasi za pembeni na ameshindwa kung'aa.Kama Moyes atamtumia Kagawa,ni dhahiri kuwa Rooney atakwenda benchi au kupelekwa nafasi nyingine.
Ferguson ndiye aliyemmaliza Shinji Kagawa kwa kumtupa benchi msimu wote wa mwaka jana na ndiyo maana,hata anapopewa nafasi kidogo,hana jipya.Kama David Moyes atampa nafasi Kagawa na kumuweka nje Rooney,hata mimi nitamuona "chizi",hata wewe utamuona "chizi" na kuna uwezekano mkubwa,hata yeye mwenyewe Moyes,atajiona "chizi" Huu ni muda wa Kagawa kutafuta mlango wa kutokea.
HII NI SEHEMU YA HOTUBA YA SIR ALEX FERGUSON ALIPOKUWA ANAWAAGA MASHABIKI WA UNITED PALE OLD TRAFFORD tarehe 12/05/2013.
"Ningependa kuwakumbusha kuwa,tulipokuwa kwenye hali ngumu,klabu ilisimama upande wangu,wafanyakazi wengine nao waliniunga mkono,wachezaji waliniiunga mkono.Jukumu lenu kwa sasa,ni kumuunga mkono kocha wetu mpya atakayekuja.Jambo hili ni la msingi sana."
"Lakini wakati ukitafakali hilo,kuna ushindi wa dakika za majeruhi,kusawazisha na hata vipigo,haya yote ni sehemu ya klabu yetu hii kubwa" alisema Ferguson.
Ron Atkinson alikuwa kocha wa Man United kuanzia mwaka 1981-1986 na katika kipindi chake chote,alifanikiwa kuwapatia United mataji mawili tu ya FA.Ferguson kwenye msimu wake wa kwanza 1986/1987 United walimaliza msimu wakiwa nafasi ya 11 na kwenye msimu wa 1989/1990 United walimaliza wakiwa nafasi ya 13.Baada ya hapo,gari likawaka na mpaka anakuja kustaafu,ametangazwa kama kocha mwenye mafanikio zaidi katika historia ya ligi kuu nchini Uingereza.Kuna mtu anajali United kumaliza nafasi ya 13 msimu ule tena?
Sisemi kuwa na Moyes naye lazima atafanikiwa,hapana.Ninachokisema ni kwamba,anahitaji muda na kutengeneza timu yake ndipo apimwe kama kafaulu au kashindwa.Kama atapewa muda na kuungwa mkono na kila mdau wa United,timu itamuhitaji mwanamke ili aweze kueleza tatizo la mtoto "man united" liko sehemu gani.
Kama unachochote na ungependa kushirikiana na mimi,nitafute kwenye ukurasa wa Facebook kwa jina la Oscar Oscar Jr,unaweza kunipata pia kwenye whatsapp kwa namba 0789-784858 na pia,unaweza kunifuata kwenye twitter kwa jina la "soka stadium"
0 comments:
Post a Comment