ARSENAL VS MAN CITY HAKUNA MBABE.
Manchester City walipoteza nafasi ya kupaa kileleni katika ligi ya Premier ya Uingereza baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Arsenal kwenye mechi ngumu iliyosakatwa kwenye uwanja wa Emirates, Jumapili.
City wangenig'atua Chelsea kutoka kileleni kwa idadi ya mabao lakini wanasalia nafasi ya tatu baada ya kiungo Mathieu Flamini kusawazisha katika kipindi cha pili baada ya David Silva kuwapa wageni uongozi katika cha kwanza.
Kufuatia siku ya kukata na shoka katika shindano hilo, alama nne pekee ndizo mwanya baina ya timu nne za kwanza huku Arsenal, walionesha ujasiri mkubwa baada ya kucharazwa 6-0 na Chelsea wikendi iliyopita.
Liverpool, walioko nafasi ya pili, watachukua hatamu za uongozi ikiwa wataweza kuwatoa manyoya wageni wao Tottenham Hotspurs huku City wakiwa na mechi mbili za ziada kwa washindani wao wa karibu.
Baada ya kiungo Tomas Rosicky kuona maombi yake ya kupewa penalti yakikataliwa dakika za mwanzo mwanzo kwa upande wa Arsenal, City walichukua uongozi dakika 18 zilipokatika pale Silva alipoelekeza boli wavuni baada ya mkwaju mkali wa mwenzake Edin Dzeko kudunda kutoka mlingoti wa lango.
Arsenal walinusurika aibu pale beki wao, Per Metersecker alipoelekeza mpira langoni mwake lakini ulikosa kuishia wavuni kwa inchi chache kipindi cha pili kilipoanza.
Dakika chache baadaye, mambo yalikuwa 1-1 pale Lukas Podolski alipopewa nafasi ya kupeperusha krosi kutoka kushoto na mwenzake Flamini aliufikia na kuachilia kombora lilomfanya kipa wa City, Joe Hart, asalimu amri.
Hart aliiokoa timu yake pale Podolski alipoachilia mzinga mzito uliopata ufundo wa mguu wa mlinda lango huyo na kutoka nje kabla ya nyota Yaya Toure, kukosa nafasi ya kupatia wageni alama zote tatu baada ya kuzuiwa na maabeki wa Arsenal hatua chache kutoka langoni.
0 comments:
Post a Comment