kapombe afanya kweli ufaransa
BEKI nyota wa Simba, Shomari Kapombe, ameonyesha kweli ana kipaji baada ya kufuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Kapombe mwenye umri wa miaka 21, amefuzu kucheza soka katika timu mbili za hapa Ufaransa.
SOKA STADIUM inaendelea kuranda nchini Ufaransa, limepata taarifa hizo za uhakika mjini hapa, lakini wakala wake, Dennis Kadito, ameendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwetu.
“Kweli Kapombe amefanya vizuri sana, amefanya majaribio hapa na timu ya As Cannes ambayo ni kubwa kabisa na nyingine (ambayo hakuitaja) lakini baada ya mawakala wa timu ya Nice kumuona nao wamepiga simu na kutaka kumsajili, amefanya vizuri sana labda kama itatokea ishu nyingine lakini kwenye majaribio amekuwa gumzo.
“Kama unavyoona hali ya hewa hapa Ufaransa kwa sasa ni nzuri na hakuna tofauti na Dar es Salaam, hivyo imekuwa bahati kwake.
“Alianza mazoezi Jumanne iliyopita baada ya kutoka Uholanzi na baadaye akahamia nyingine na zote amefuzu. Jamaa walimchezesha beki wa kushoto kwa dakika 15, wakaona uwezo wake, baadaye wakamhamishia namba sita na huko akacheza vizuri zaidi,” alisema Kadito na alipoulizwa kuhusu dau, akasema:
“Hapo kidogo inabidi nizungumze na Simba, unajua tunapata tatizo kutokana na Tanzania kutokuwa na jina katika soka la kimataifa. Hivyo nitazungumza na uongozi wa klabu yake na ninyi mtapata taarifa.”
Pamoja na kuwa mgeni katika soka la Ulaya, Kapombe alionyesha uwezo mkubwa na kuwashangaza baadhi ya mawakala wengine ambao walialikwa kwa ajili ya kumwangalia huku wengi wakijaa wakati alipofanya majaribio Cannes kwa kuwa ni timu maarufu sana hapa Ufaransa.
Utulivu wake kwenye mpira, pasi za uhakika na ujuzi wa kukaba, zilionyesha kuwavutia mawakala wengi kutoka sehemu mbalimbali waliokuwa wakimuangalia katika majaribio nchini Uholanzi tangu alipotua zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Suala la Tanzania kutokuwa maarufu kisoka, huenda ndiyo limekuwa hofu kwao lakini tayari Kapombe amemaliza kazi yake, kilichobaki ni makubaliano tu kati ya klabu itakayomtaka na Simba.
SOKA STADIUM inaendelea kuranda anga hizi huku likifuatilia zaidi kujua kuhusiana na mchezaji huyo kinda Mtanzania ambaye kama atapata nafasi, huenda akawa amewasaidia Watanzania wengine kutoka.
0 comments:
Post a Comment