Pacha kutoka Ivory Coast, Kipre Balou na Kipre Tchetche waliopishana msimu mmoja kuingia Azam nao wameongeza miaka miwili kila mmoja. Balou atakuwa mali ya timu ya Bilionea Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa hadi mwaka 2016, wakati Kipre hadi 2015.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrisa Mohamed ‘Father’ amezungumza mchana huu kwamba, uongozi wa klabu kwa kuzingatia ubora wa wachezaji hao, umeamua kuwaongezea Mikataba.
“Wazi tuna muda mrefu zaidi wa kuendelea kuhitaji huduma ya wachezaji bora kama hawa. Unapozungumzia watu kama Sure Boy, Kipre Tchetche na Kipre Balou, hawa ni wachezaji wakubwa sana katika Ligi ya Tanzania. Huwezi kuthubutu kuwa nao kwa Mkataba wa muda mfupi. Hizi ni bidhaa adimu,”alisema.
Sure Boy ni kati ya wachezaji wanne tu waliobaki kati ya waliopandisha Azam Ligi Kuu mwaka 2008, wengine wakiwa ni John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Luckson Kakolaki na Malika Philip Ndeule.
Alijiunga na Azam FC mwaka 2006 ikiwa Daraja la Kwanza akitokea timu ya mtaani, Friends Rangers ya Manzese na sasa ni kati ya wachezaji tegemeo wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Azam FC imekuwa ikipokea ofa kadhaa kutoka klabu mbalimbali barani, ikiwemo El Hilal ya Sudan kutaka kumnunua Sure Boy, lakini imekuwa ikikataa kwa matumaini ya kumuuza Ulaya baadaye.
Tchetche alitangulia kujiunga na Azam mwaka 2010 kabla ya msimu uliofuata kufuatiwa na pacha wake, Balou na wote klabu ilivutiwa nao walipokuja na timu ya taifa ya vijana ya Ivory Coast kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka 2010 Dar es Salaam kama waalikwa wa kunogesha mashindano.
Tchetche aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita kwa mabao yake 16 na mdogo wake, Balou kwa pamoja na Sure waliifanya Azam iwe na safu imara mno ya kiungo hadi kuukosa kosa kidogo tu ubingwa wa Ligi Kuu, ikizidiwa kete na Yanga SC.
Katika hatua nyingine, Nassor amesema Azam FC ambayo kwa takriban wiki nzima sasa imekwishaanza maandalizi ya msimu mpya, Jumanne itacheza mchezo wa kirafiki na kombaini ya timu za Majeshi ya Kujenga Taifa (JKT) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika sherehe za miaka 50 ya jeshi hilo.
Muungano wa wachezaji kutoka JKT Oljoro, JKT Mgambo, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zote za Ligi Kuu dhidi ya washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam FC hakika itakuwa mechi tamu Jumanne.
0 comments:
Post a Comment