JUMA KASSEJA HAKUTAKA KUZUNGUMZA NA CLUB YAKE YA SIMBA
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba Juma Kaseja hakutaka kukutana na uongozi wa klabu hiyo kujadiliana juu ya mustakabali wake, licha ya kuitwa kwa miezi miwili na ndiyo maana wakaamua kuachana naye.
Akizungumza asubuhi ya leo, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Poppe amesema kwamba tangu Mei wamekuwa wakimuita Kaseja kwa ajili ya mazungumzo juu ya mustakabali wake katika klabu hiyo, lakini amekuwa akipiga chenga.
Poppe alisema mara ya mwisho kukutana ana kwa ana na Kaseja ni wakati wakiwa Morocco na timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi ya wenyeji kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mapema mwezi huu.
“Nilipokutana naye, nikamuambia sisi bado tuna nia ya kuendelea na wewe, je wewe msimamo wako ni upi? Akasema hawezi kujibu kwa sababu ana majukumu ya timu ya taifa, akimaliza atajibu. Nikamuambia sawa, wewe maliza na ukiwa tayari njoo ofisini tuzungumze.
Amemaliza mechi na Morocco, wamerudi hapa, amecheza mechi na Ivory Coast amemaliza na wiki zaidi ya mbili zimepita hajaja. Sisi tukaona huyu mtu kwa kuwa amemaliza Mkataba wake hapa na tunamuita haji, anaweza kuwa na mipango yake mingine, tumuache aendelee nayo,”alisema Poppe.
Alipoulizwa kuhusu kuachwa kwa sababu ameshuka kiwango, Poppe alisema; “Ni kweli kama utaona udakaji wake wa sasa, ameshuka mno kiwango na hilo linatupa wakati mgumu sana mbele ya mashabiki. Na kama utakumbuka Morogoro walitaka kumpiga.
Sasa ukitazama kwa mfano lile bao la kwanza alilofungwa katika mechi na Yanga, lilikuwa bao rahisi sana. Ule mpira ulipita mbele yake ukaenda kupigwa kichwa (na Didier Kavumbangu). Sasa ile kwa kweli imewaudhi sana watu,”.
“Lakini pamoja na yote, tulitaka tuzungumze naye mwenyewe, tujadiliane juu ya hali halisi, ikibidi hata kumsainisha Mkataba na kumpa fedha anazotaka, kisha tumpe mapumziko ya muda fulani, ili awe fiti arudi kazini. Lakini hakutupa fursa hiyo. Tungefanya nini?,”alihoji Hans Poppe.
Askari huyo wa zamani amesema kwamba Kaseja kama angejitambua yeye ni gwiji wa klabu, asingethubutu kupiga chenga kikao na uongozi, hususan katika kipindi hiki kigumu ambacho klabu inahitaji kujipanga upya baada ya msimu mbovu uliopita ikipoteza taji la ubingwa wa Ligi Kuu.
“Mwisho kabisa, tukaamua kumteua mtu maalumu wa kuzungumza naye, Evans Aveva. Aveva kila akimpigia simu Kaseja, anatoa udhuru, mara yuko Kigoma, mara yupo Korogwe, sasa mtu kama huyu sisi tungefanya nini?”alihoji tena Poppe.
"Na pia huyu mtu kama maslahi katika klabu hii amepata makubwa kwa sababu alikuwa anathaminiwa mno. Juma Kaseja ni kati ya wachezaji ambao watastaafu soka vizuri tu. Amevuna fedha nyingi sana hapa. Wakati wote yeye alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi kwa upande wa wazawa. Na unapofika wakati wa usajili, alikuwa anapiga hela ndefu sana hapa,"alisema Poppe.
Historia ya Kaseja na Simba SC imefikia tamati mapema wiki hii, baada ya klabu kuamua kutomuongezea Mkataba kipa huyo iliyemsajili mwaka 2003 kutoka Moro United ya Morogoro.
Kaseja amekaririwa na gazeti la Serikali, Habari Leo akisema kwamba atawaaumbua viongozi wa Simba SC kwa kuanika kila kitu baada ya kutemwa. Lakini anapotafutwa na vyombo vingine vya habari, amekuwa akikataa kuzungumzia sakata hilo.
0 comments:
Post a Comment