Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 January 2015
Friday, January 16, 2015

Uchambuzi: Stand United vs Azam Fc. Kambarage Stadium




Na Oscar Oscar Jr

Bingwa mtetezi wa ligi kuu Tanzania bara, Azam Fc leo watakuwa ugenini kucheza na timu ya Stand United kwenye uwanja wa Kambarage kule mkoani Shinyanga mchezo utakaopigwa majira ya saa 10:30 Jioni. 

Azam ambao wanakamata nafasi ya nne wakiwa na alama 14, watakuwa na kibarua kizito kwa wakatatishaji tiketi hao wa kituo cha mabasi pale Shinyanga hasa ukizingatia kuwa wana hamu ya kupata pointi tatu mbele ya timu "kigogo"

Stand United tayari wamefanikiwa kupata alama tatu mbele ya timu bora ya Mbeya City na kutoka sare na timu ya Simba, rekodi hii inaweza kuwa chachu kwa wao kupambana na kuhakikisha wanaondoka na alama tatu mbele ya wana lamaba lamba hao ambao wameshapoteza mechi mbili msimu huu.

Azam Fc ambao walitolewa kwenye michuano ya Mapinduzi kwenye hatua ya robo Fainali, bado tatizo linaendelea kubaki kwenye benchi la ufundi ambalo mpaka sasa, wanaonekana kubabaika na kushindwa kupata kikosi cha kwa kwanza.

Kocha Joseph Omog amekuwa akishindwa kuamua nani awe kipa wa kwanza kati ya Aishi Manula na Mwadini Ally. Hawa magolikipa wamekuwa wakipokezana kila siku kitu ambacho kinawanyima mechi za kutosha na hivyo kupunguza uwezekano wa kipa mmoja kuwa bora zaidi ya mwenzie.

Stand United ambao wanakamata nafasi ya 10 wakiwa na pointi 11, bado hawako mahali salama na watahitaji ushindi kwenye mchezo wa leo hasa ukizingatia tofauti iliyopo baina yao na Tanzania Prisons ambao wanashika nafasi ya mwisho ni alama nne pekee.

Kwa upande wa Azam ambao wanajiandaa pia kwa michuano ya klabu bingwa Afrika, wanahitaji kupata ushindi ili kuongeza hali ya kujiamini kwa wachezaji na benchi la ufundi lakini pia, wanahitaji kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi ili kujihakikishia utetezi wa kombe hilo ambalo walilitwaa kwa mara ya kwanza msimu 
uliopita.

Kwa muda sasa Azam imekuwa ikiwatumia Agrey Morris, Said Morad na David Mwantika kama walinzi wa kati lakini ujio wa Pascal Wawa ambaye ameonekana bado hajazoeana na wenzie vizuri, umewafanya Azam kupoteza sifa ya kuwa timu yenye safu bora ya ulinzi.

Endapo Azam wataibuka na ushindi kwenye mchezo huo, wanaweza kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu lakini kama watapoteza, upo uwezekano wakushuka hadi kwenye nafasi ya 10. 

Stand United ambao wameshafungwa na Yanga kwenye uwanja huo, wakipata ushindi wanaweza kupanda hadi kwenye timu tano za juu ingawa safu yao ya ulizi inakamata nafasi ya pili kwa ubovu baada ya Ndanda Fc ambao wameruhusu mabao 14, wao wameruhusu 11.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!