Searching...
Image and video hosting by TinyPic
17 January 2015
Saturday, January 17, 2015

Uchambuzi: Ndanda fc vs Simba Sc. Nangwanda Stadium



Na Oscar Oscar Jr

Mabingwa wa Mapinduzi Cup timu ya Simba, leo itashuka dimbani ugenini kule mkoani Mtwara kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kupambana na wenyeji timu ya Ndanda Fc. 

Simba ndiyo timu pekee iliyokwenda kwenye michuano ya Mapinduzi kutoka Tanzania bara huku ikipewa nafasi finyu ya kufanya vizuri lakini kwa mshangao wa walio wengi, waliibuka Mabingwa kwa mikwaju ya Penalty dhidi ya Mtibwa Sugar.

Simba ambao wamepata sare michezo sita, kushinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja, wanaonekana kujiamini zaidi chini ya kocha mpya Goran Kopunovic aliyechukuwa mikoba ya Patrick Phiri kwenye michuano ya Mapinduzi na watu wengi wanataka kuona kama moto wa Mapinduzi watauleta pia kwenye ligi kuu ya Vodacom.

Kwa upande wa Ndanda Fc chini ya kocha mpya Abdul Mingange, nao wanaonekana kuimarika na katika michezo yao miwili ya hivi karibuni hawajapoteza hata mmoja huku wakishinda dhidi ya Tanzania Prisons ugenini kabla ya kutoka sare ya Polis Morogoro wakiwa nyumbani.

Simba wanapaswa kuwa watulivu kwenye mchezo huu na kuwaheshimu Ndanda Fc ambao pamoja na kushika nafasi ya 11 kwenye ligi kuu, tayari walifanikiwa kuwafunga Azam Fc ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo ndani ya dimba ambalo Simba pia atashuka dimbani leo hii majira ya saa 10: 30 Jioni.

Ndanda Fc ambao wamefungwa mabao 14 mpaka sasa, watakuwa na mtihani mkubwa pale watakapokutana na washambuliaji wa Simba hatari kama Emmanuel Okwi na Danny Sserunkuma ambao wanatarajiwa kuanzishwa kwenye mchezo wa leo.

Ndanda Fc ambao wamekusanya alama 11 wanahitaji kupigana ili kujikusanyia alama nyingi kabla ya mechi za mwisho ambazo huwa zimejaa upinzani hasa ukizingatia kuwa kutakuwa na timu zinazopigania ubingwa na zile zinazokwepa kushuka daraja.

Kwa upande wa Simba endapo watapata ushindi, wanaweza kufufua matumaini ya kupigania nafasi moja kati ya mbili za juu kwani watatimiza alama 12 na kuweza kupanda juu kwenye msimamo wa ligi kuu ambayo Mtibwa Sugar ndiyo vinara wakiwa na alama 16.

Kuelekea mchezo wa leo, Simba wanakamata nafasi ya 12 huku wakiwa wamefunga mabao saba na kufungwa saba wakati Ndanda Fc, wao wanakamata nafasi ya 11 wakiwa wamefungwa mabao 14 na kufunga mabao tisa lakini, wamecheza michezo 10 wakati Simba wameshuka dimbani mara nane pekee.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!