Searching...
Image and video hosting by TinyPic
16 January 2015
Friday, January 16, 2015

Uchambuzi: kuelekea mechi ya Yanga vs Ruvu Shooting.


Na Oscar Oscar Jr

Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania bara, timu ya Yanga leo watashuka dimbani kwenye uwanja wa Taifa majira ya saa 10:30 kuvaana na Ruvu Shooting kwenye muendelezo wa mechi za ligi kuu.

Hii ni baada ya michuano ya mapinduzi kumalizika kule visiwani Zanzibar huku Yanga walioshiriki wakiondoshwa kwenye michuano hiyo katika hatua ya robo fainali pengine kinyume na matarajio ya watu wengi.

Ruvu Shooting ambao tayari wameshuka dimbani mara tisa, wamefanikiwa kukusanya alama 11 na kukamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi kuu. 

Bado tatizo kubwa la timu hii ya kocha Tom Olaba, linaonekana kuwa kwenye safu ya ushambuliaji ambapo mpaka sasa wamefunga mabao matano pekee.

Ruvu Shooting ambao wametoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Mgambo JKT kule jijini Tanga, wanakutana na Yanga huku wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa bao 7-0 na timu hiyo msimu uliopita. 

Hii ni mechi nyingine tofauti na itakuwa na presha tofauti hasa ukizingatia kuwa, Yanga wana kiu ya kuwafurahisha mashabiki wake baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye michuano ya Mapinduzi. 

Kwa upande wa vijana wa kocha Tom Olaba, wanaweza wasiwe na presha yoyote kwa sababu hata matokeo ya sare kwao yanaweza yasiwaathiri chochote hasa ukizingatia kuwa alama moja inawawezesha kutimiza alama 12 na kusogea katikati mwa msimamo wa ligi hiyo.

Yanga ambao wana alama 14, watakuwa na shughuri pevu kwani tayari timu za Mtibwa Sugar na JKT Ruvu ziko kileleni na alama 16 na hivyo ushindi pekee kwenye mchezo huo ndiyo utakao waweka kwenye mbio hizo za kuusaka ubingwa.

Ujio wa Kocha Hans Van Der Pluijm umeleta mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga huku Simoni Msuva akionekana kuanza na Mrisho Ngassa akitokea benchi.

Kwenye safu ya ushambuliaji, bado Kpah Shermann na Amis Tambwe wanaweza kuanza katika eneo hilo la kutikisa ukuta wa Ruvu Shooting ambao wameruhusu mabao saba mpaka sasa.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!