Searching...
Image and video hosting by TinyPic
25 December 2014
Thursday, December 25, 2014

Uchambuzi: Chelsea vs West Ham


Na Chikoti Cico

Ligi kuu nchini Uingereza itaendelea tena Ijumaa ya wiki hii maarufu kama siku ya “boxing day” ambapo katika uwanja wa Stamford Bridge timu ya Chelsea itaikaribisha West Ham katika moja ya mechi inayotarajiwa kuwa ya kusisimua.

Chelsea ambao wanashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 42 baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Stoke City kwa magoli 2-0 wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo wakiwa na ari ya kutaka kuendelea kujikita kileleni.

Kocha wa Chelsea Jose Mourinho anaweza kumkosa kiungo wake mahiri Eden Hazard ambaye aliumia kwenye mchezo dhidi ya Stoke lakini Oscar ambaye hakucheza mchezo huo anaweza kurejea kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya West Ham.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha Chelsea wamekuwa na rekodi nzuri kwa mechi zinazochezwa siku ya “Boxing day” kwani katika michezo tisa iliyopita wameshinda michezo mitano na kutoka sare michezo minne huku wakiwa hawajafungwa mchezo wowote.

Kikosi cha Chelsea kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Cahill, Terry, Azpilicueta; Fabregas, Matic; Willian, Oscar, Hazard; Costa

Nao West Ham ambao wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 31 baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Leicester City wanatarajiwa kuleta upinzani mkubwa dhidi ya Chelsea hasa ikizingatiwa kwamba nao wanataka kubaki “top four”.

Kocha wa West Ham Sam Allardyce kuelekea mchezo huo atamkosa James Tomkins ambaye ni majeruhi huku kiungo Mark Noble ambaye alikosa mechi nne zilizopita kutoka na kuwa majeruhi akitarajiwa kucheza mchezo huo dhidi ya Chelsea huku James Collins akitarajiwa kucheza sambamba na Winston Reid kwenye eneo la ulinzi.

Sam Allardyce kocha wa West Ham anaonekana kuwa na rekodi mbovu dhidi ya Chelsea kwani takwimu zinaonyesha katika michezo 21 aliyocheza dhidi yao ameshinda michezo miwili tu huku akifungwa michezo 13 na kutoka sare michezo sita.

Pia West Ham wanaonekana kuwa na rekodi mbaya dhidi ya Chelsea kwani katika michezo 16 iliyopita waliyocheza nao wameshinda mchezo mmoja tu na kufungwa michezo 12 huku wakitoka sare michezo mitatu.

Kikosi cha West Ham kinaweza kuwa hivi: Adrian, Jenkinson, Tomkins, Reid, Cresswell, Song, Kouyate, Nolan, Downing, Valencia, Carroll

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!