Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 January 2015
Wednesday, January 28, 2015

Ni Ghana na Algeria kundi C.




Na Chikoti Cico


Timu ya taifa ya Ghana na Algeria zimefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali kwenye michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika yanayoendelea nchini Guinea ya Ikweta baada ya kushinda michezo yao ya mwisho ya kundi C.

Ghana waliokuwa wanacheza na Afrika ya Kusini katika kumalizia mchezo wa tatu na wa mwisho wa kundi C maarufu kama “kundi la kifo” waliweza kuibuka na ushindi wa magoli 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Estadio di Mongomo.

Magoli ya John Boye kwenye dakika ya 73 ya mchezo na Andrew Ayew dakika ya 83 yaliiwezesha Ghana kunyakua alama zote tatu na kuvuka hatua ya makundi huku goli la kufutia machozi la Afrika ya Kusini maarufu kama Bafana Bafana likifungwa na Mandla Masango kwenye dakika ya 17 ya mchezo.

Kwa matokeo hayo Ghana imefikisha alama sita na kuongoza kundi C na hivyo kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali huku timu ya Afrika Kusini ikiyaaga mashindano hayo baada ya kushika mkia kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na alama moja.

Mchezo mwingine wa kundi C ulikuwa ni kati ya Algeria dhidi ya Senegal mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Estadio de Malabo ambapo uliisha kwa matokeo ya magoli 2-0 ambapo Algeria walishinda mchezo huo.

Magoli ya Riyad Mahrez kwenye dakika ya 11 ya mchezo na Nabil Bentaleb dakika ya 82 yaliihakikishia ushindi timu ya taifa ya Algeria na hivyo kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi C wakiwa na alama sita hivyo kufuzu kwa hatua ya robo fainali.

Senegal ambao walihitaji sare tu ili kuweza kuvuka hatua ya makundi, kwa matokeo hayo dhidi ya Algeria wameyaaga mashindano ya AFCON baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi C wakiwa na alama nne.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!