Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 January 2015
Wednesday, January 28, 2015

Ni Chelsea Wembley.




Na Chikoti Cico



Ulikuwa mchezo wa Machozi Jasho na Damu, kila timu ilipigana kutafuta ushindi na kila timu ilitaka kufika Wembley ulikuwa mchezo bora ambao usingedhani kama ni nusu fainali bali fainali. 

Kwa maneno machache hivyo ndivyo unavyoweza kusema kuhusu mchezo wa nusu fainali ya pili ya kombe la Capital One kati ya Chelsea dhidi ya Liverpool iliyochezwa usiku wa Jumanne kwenye uwanja wa Stamford Bridge.

Mchezo huo ulioanza saa 4:45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ulishuhudia Liverpool wakionyesha kandanda safi na kukosa nafasi nyingi za wazi kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Raheem Sterling na Philipe Coutinho.

Huku kikwazo kikubwa kwa timu ya Liverpool akiwa ni kipa wa Chelsea Thibaus Courtois ambaye aliokoa michomo mingi iliyokuwa inaelekezwa golini kwake kwa sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza.

Lakini pia timu ya Chelsea ilitengeneza nafasi chache za magoli kwa kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake Diego Costa ambaye alikuwa akisumbuana na beki wa Liverpool Martin Skrtel katika matukio tofauti tofauti uwanjani. 

Huku katika tukio la dakika ya 11 Costa alionekana kumkanyaga beki wa Liverpool, Emre Can akiwa hana mpira ingawa mwamuzi hakuweza kuona tukio hilo ambalo lingepelekea mchezaji huyo kuonyeshwa kadi nyekundu.

Pia kwenye dakika ya 22 Skrtel alionekana kumwangusha Costa kwenye eneo la hatari ingawa mwamuzi wa mchezo huo Michael Oliver hakutoa penati tukio lililopelekea kocha wa Chelsea Jose Mourinho kubaki akilalamika kwa kamisaa wa mchezo huo Phil dowd.

Hivyo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake na kufanya matokeo ya jumla (aggregate) ya nusu fainali ya kwanza kuendelea kubaki kuwa 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Chelsea wakionekana kuliandama zaidi lango la Liverpool kupitia kwa Willian na Eden Hazard ambao waliisumbua sana ngome ya Liverpool kwa chenga na pasi fupi fupi za haraka ingawa juhudi zao hazikuweza kuzaa matunda.

Pamoja na mashambulizi ya hapa na pale kutokea kwa timu zote mbili kwenye kipindi cha pili lakini mpaka dakika 90 mchezo huo zinamalizika hakuna timu iliyoweza kuondoka na ushindi.

Iliwachukua Chelsea mpaka dakika ya 94 ya muda wa nyongeza (extra time) wa dakika 30 kuweza kupata goli kupitia kwa Ivanovic aliyeunganisha kwa kichwa mpira mdogo wa adhabu uliopigwa na Willian.

Liverpool ambao walionekana kuchoka baada ya kuongezwa dakika hizo 30 walijitahidi kurejesha goli hilo moja lakini mpaka mwamuzi wa mchezo huo anapuliza kipyenga kuashiria kumalizika kwa mchezo walikuwa ni Chelsea walioweza kuibuka na ushindi na hivyo kuingia fainali ya Capital One itakayochezwa kwenye uwanjwa wa Wembley.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!