Na Chikoti Cico.
Viwanja mbalimbali nchini Uingereza vitawaka moto wikendi hii huku kwenye uwanja wa St James Park timu ya Newcastle United itaikaribisha Chelsea mchezo utakaopigwa saa 9:45 kwa saa za Afrika Mashariki na mwamuzi wa mchezo huo ni Martin Atkinson.
Timu ya Newcastle United inayofundishwa na kocha Alan Pardew baada ya kutoka sare na kufungwa michezo miwili iliyopita, wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo dhidi ya Chelsea kwa nguvu zote ili kutafuta alama tatu muhimu na kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.
Ikiwa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo ikiwa na alama 20, timu ya Newcastle itawakosa Siem de Jong, Davide Santon, Gabriel Obertan, Ryan Taylor, Tim Krul na Sammy Ameobi ambao ni majeruhi ila kurejea kwa Moussa Sissoko na Jack Colback ambao walikuwa wanatumikia adhabu kutaiongezea nguvu timu hiyo dhidi ya Chelsea.
Kikosi cha Kocha Pardew kinaweza kuwa hivi: Elliot; Janmaat, Taylor, Dummett, Haidara; Colback, Tiote; Gouffran, Sissoko, Perez; Cisse
Kuelekea mchezo huo dhidi ya Newcastle, vinara wa ligi kuu nchini Uingereza timu ya Chelsea inayofundishwa na kocha Jose Mourinho itamkosa kiungo mahiri wa ukabaji Nemanja Matic ambaye atakuwa nje kutumikia adhabu ya kuonyeshwa kadi tano za njano hivyo kati ya Ramirez ama Mikel mmoja ataziba nafasi ya Matic.
Mpaka sasa Chelsea inashika nafasi ya kwanza ikiwa na alama 36 kwenye msimamo wa ligi huku wakiwa wamecheza michezo 14 bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Rekodi hii Mourinho atatamani kuiendeleza kwa kuifunga Newcastle United. Wakati huo huo mshambuliaji wa Chelsea, Diego Costa atarejea uwanjani baada ya kumaliza adhabu ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Spurs.
Takwimu za mchezo huo zinaonyesha kuwa, mara nne Jose Mourinho alizocheza na Newcastle ugenini ameshindwa kupata ushindi hata mmoja huku akifungwa mara mbili na kutoka sare mara mbili.
Pia takwimu zinaonyesha kiungo wa Chelsea Eden Hazard, amefunga magoli manne kati ya mara mechi tatu alizocheza dhidi ya Newcastle United.
Kikosi cha kocha Mourinho kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Cahill, Terry, Azpilicueta; Mikel, Fabregas; Hazard, Oscar, Willian; Costa.
Rekodi zinaonyesha katika michezo 138 ya ligi waliyokutana Newcastle na Chelsea, Newcastle ameshinda michezo 47 huku Chelsea akishinda michezo 55 na wametoka sare michezo 36.
0 comments:
Post a Comment