Searching...
Image and video hosting by TinyPic
6 December 2014
Saturday, December 06, 2014

Uchambuzi: Manchester City vs Everton


Na Chikoti Cico

Uwanja wa Etihad jijini Manchester utawaka moto wikendi hii kwa timu ya Manchester City kuialika Everton katika mchezo unaotarajiwa kuwa wakupiga nikupige katika kutafuta alama tatu.

Andre Marriner ndiye mwamuzi atayesimamia mchezo huo utakaopigwa saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Timu ya Manchester City inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na mfululizo wa matokeo mazuri baada ya kushinda mechi nne zilizopita katika mashindano mbalimbali hivyo ari ya timu hiyo imerejea katika kuifukuzia timu ya Chelsea inayoongoza ligi hiyo.

Mpaka sasa City inayofundishwa na kocha Manuel Pellegrini inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 30, kuelekea mchezo huo City itawakosa Vicent Kompany, David Silva ambao ni majeruhi.

Mshambuliaji, Stevan Jovetic akitarajia kupumzishwa kama tahadhari baada ya kupata maumivu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sunderland.

Wachezaji ambao walikuwa majeruhi kwa muda mrefu mshambuliaji Edin Dzeko na beki Aleksandar Kolarov wanaweza kucheza dhidi ya Everton baada ya kupona huku pia beki Eliaquim Mangala akirejea kikosi baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo dhidi ya Southampton.

Kuelekea mchezo huo takwimu zinaonyesha mshambuliaji wa City Sergio Aguero katika michezo nane iliyopita aliyocheza Etihad amefunga magoli saba huku mpaka sasa akiwa na magoli 14 kwenye ligi kuu nchini Uingereza.

Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Mangala, Demichelis, Clichy; Navas, Toure, Fernandinho, Nasri; Dzeko, Aguero.

Kwa upande wa kocha wa Everton Roberto Martinez kuelekea mchezo huo atawakosa Steven Naismith, James McCarthy, John Stones na Darron Gibson ambao ni majeruhi.

Beki Antolin Alcaraz ataweza kurejea kikosini kwenye mchezo huo baada ya kukosa michezo sita katiika mashindano mbalimbali baada ya kuumia bega.

Wakiwa na alama 18 Everton wanashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi baada ya kupata alama moja tu kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Spurs na Hull City hivyo mchezo dhidi ya City watahitajika kushinda ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.

Wakati huo huo kocha wa Everton Martinez amekuwa hana rekodi nzuri dhidi ya Manchester City kwani katika michezo 10 aliyocheza nao akiwa kocha amefungwa michezo tisa na kutoka sare mchezo mmoja.

Kikosi cha Everton kinaweza kuwa hivi: Howard; Coleman, Jagielka, Distin, Baines; Besic, Barry; Mirallas, Barkley, Pienaar; Lukaku.

Takwimu kiujumla zinaonyesha katika michezo 162 ambayo Manchester City wamekutana na Everton, City wameshinda michezo 61 huku pia Everton akishinda michezo 61 na wametoka sare michezo 40.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!