Searching...
Image and video hosting by TinyPic
10 December 2014
Wednesday, December 10, 2014

NIONAVYO MIMI: TATIZO NI NAFASI YA DAVID DE GEA.


Na Oscar Oscar Jr

Ukiambiwa utaje mchezaji bora wa ligi kuu nchini Uingereza mpaka sasa, huwezi kukosa jibu. Wapo watakao kwambia ni Sergio Kun Aguero ambaye ameshafunga magoli 14, wapo wengine watakwambia ni Diego Costa ambaye ameshafunga magoli 11 na kuifanya Chelsea kubakia kileleni.

Kwa upande mwingine, utakutana na kundi ambalo litamtaja Cesc Fabregas ambaye mpaka sasa ndiye kinara wa pasi za mwisho, wapo pia watakaotaja jina la Alexies Sanchez. Unajua sababu? magoli yanahisia za ndani zaidi kuliko chochote kwenye mchezo wa soka.

Ukihitaji majina ya wachezaji wanne bora wa Manchester United msimu huu mpaka sasa, utakutana na Angel Di Maria, Wayne Rooney, Roben Van Persie na David De Gea.

Ukihitaji watatu, utakutana na Van Persie, Rooney na De Gea. Ukihitaji wawili, utaambiwa ni Rooney na De Gea. Ukiambiwa utaje mchezaji mmoja je? bila shaka jina la David De Gea litaendelea kujirudia.

Kucheza nyuma ya walinzi kama MacNair, Smalling na Blackett na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu, sio kitu kidogo. Unaweza kumleta Manuel Neuer kwenye beki ya United na akachemsha, unaweza kumleta Iker Casillas naye pia akachemsha.

Nafasi ya golikipa inavuma zaidi kwa ubaya kuliko mazuri wanayoyafanya. Huwezi kukuta watu wanajadili ubora wa golikipa wiki nzima kwa kazi aliyofanya weekend iliyopita.

kipa wa Sunderland, Vito Manone ndiye aliyekuwa na wastani mkubwa wa kuokoa mashambulizi langoni mwake msimu uliopita kuliko kipa mwingine wa EPL. Kuna mtu anakumbuka hilo? hapana.

Kinachokumbukwa zaidi ni makosa yake na yale ya beki wake Wes Brown yaliyomfanya Alexies Sanchez awafunge magoli mawili msimu huu walipocheza dhidi ya Arsenal. 

Kinachokumbukwa zaidi ni makosa yake yaliyopeleke wapate kipigo cha bao 8-0 mbele ya Southampton msimu huu! Haya ndiyo matukio ambayo hukumbukwa zaidi yapofanywa na magolikipa.

Mshambuliaji anaweza kukosa nafasi hata tano za wazi kwenye mchezo lakini anapofunga bao la ushindi hata kama ni kwa mkwaju wa Penalty, mashabiki watamtukuza wiki nzima.

Kazi anayoifanya De Gea hata kama hapigi pasi za mwisho, hata kama hafungi magoli, hata kama hapigi visigino, inapaswa kuwekwa kwenye chati za juu. 

Kazi anayofanya langoni ingekuwa ni mshambuliaji, pengine De Gea angekuwa amempita Aguero kwa magoli. Pengine angekuwa anakimbizana na Fabregsa kwa pasi za mwisho. Tatizo ni nafasi anayocheza!

Pamoja na kuwa kipa wa Ujerumani na Bayern Munich, Manuel Neuer amefanya vizuri mwaka huu, bado kupewa Ballon D'or mbele ya kina Mr. Hat-Trick (Messi & Ronaldo) ni muujiza labda wakubwa walazimishe. Tatizo ni nafasi anayocheza Neuer!

Guillermo Ochoa ni moja ya magolikipa waliofanya vizuri sana kombe la Dunia mwaka huu kule Brazil. Kuna mtu anakumbuka aliokoa michomo mingapi langoni mwake? Unadhani takwimu hazipo? 

Hii ni nafasi ambayo hata magazeti hayapendi kutoa takwimu zake, wachambuzi hawaigusii sana, wadau wala hawana habari. Anyway, mimi mwenyewe ninachokumbuka kule Brazil ni goli tu la Roben Van Persie dhidi ya Hispania.



 

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!