Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 December 2014
Tuesday, December 02, 2014

Uchambuzi: Chelsea vs Tottenham Hotspur


Na Chikoti Cico

Ligi kuu nchini Uingereza inatarajia kuendelea kutimua vumbi siku ya Jumatano ambapo kwenye uwanja wa Stamford Bridge, timu ya Chelsea itaikaribisha Tottenham Hotspur mchezo unaojulikana kama “London derby” hivyo unategemewa kuwa mchezo wa kusisimua sana.

Chelsea inayoongoza ligi hiyo ikiwa na alama 33 baada ya kupoteza alama mbili kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sunderland kwa kutoka sare ya bila kufungana, inatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo ikitaka kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kuchukua alamu tatu muhimu dhidi ya Spurs.

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho anatarajia kuingia kwenye mchezo huo akitaka kuendelea rekodi ya kutofungwa toka kuanza kwa msimu wa ligi ingawa atamkosa mshambuliaji wake Diego Costa ambaye anatumikia adhabu ya kuonyeshwa kadi tano za njano.

Mshambuliaji Loic Remy ama Didier Drogba, mmoja wao ataweza kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Chelsea.

Chelsea wanaonekana kuwa na rekodi nzuri kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stamford Bridge kwani katika michezo 34 iliyopita ya ligi wameshinda michezo 28, kutoka sare michezo mitano na kufungwa mchezo mmoja tu.

Kikosi cha kocha Mourinho kinaweza kuwa hivi: Courtois; Ivanovic, Cahill, Terry, Azpilicueta; Matic, Fabregas; Schurrle, Oscar, Hazard; Remy

Kwa upande wa timu ya Tottenham Hotspur, wao wanaingia kwenye mchezo huo dhidi ya Chelsea wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga timu ya Everton kwa magoli 2-1 kwenye mchezo uliopita wa ligi hivyo watataka kuendeleza hamasa hiyo ya ushindi kutafuta alama tatu muhimu kwenye mchezo huo.

Spurs inayofundishwa na kocha, Mauricio Pochettino mpaka sasa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 20. Kuelekea mchezo huo, bado hali za wachezaji Emmanuel Adebayor, Etienne Capoue na Danny Rose hazijafahamika kama wataweza kucheza.

Beki Kyle Naughton akitarajiwa kurejea kikosini baada ya kutumikia adhabu ya kuwa nje kwa mechi mbili.

Takwimu zinaonyesha Spurs hawajawahi kushinda kwenye uwanja wa Stamford Bridge toka mwaka 1990 huku katika michezo 27 iliyocheza dhidi ya Chelsea, imefungwa michezo 17 na kutoka sare michezo 10.

Pia takwimu zinaonyesha katika michezo sita iliyopita ya ugenini kwenye ligi kuu, Spurs wameshinda michezo mitatu, kutoka sare michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja peke yake.

Kikosi cha Kocha Pochettino kinaweza kuwa hivi: Lloris; Naughton, Vertonghen, Fazio, Davies; Lennon, Bentaleb, Mason, Eriksen; Kane, Soldado

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!