Searching...
Image and video hosting by TinyPic
25 November 2014
Tuesday, November 25, 2014

Vipaji vya watanzania vinavyopotea!


Na Samuel Samuel

Wakati kaka yangu Method Mogella akiiacha Simba SC na kutua Jangwani , aliacha vilio na machungu mengi sana kwenye timu hiyo yenye masikani yake mitaa ya Msimbazi jijini Dar Es Salaam. 

Wapo waliodiriki kuacha kabisa kushabikia soka na wengine kujenga chuki kabisa kwa mkongwe huyo ambaye alikuwa anaimudu vyema nafasi ya kiungo mkabaji na beki wa kati. Kuna mambo ambayo yaliwafanya mashabiki wa timu hiyo kufikia hatua hiyo. 

Marehemu Method aliijua kazi yake na kwa zaidi ya miaka mitatu alisimama kama nguzo imara kwa Simba SC kabla ya December 1993, kuikacha timu hiyo na kuhamia Yanga kama beki namba nne akishirikiana vyema na wakongwe Keneth Mkapa, Ngadou Ramadhani na Costantine Kimanda. 

Nataka kusema nini, Mogella na hata Akida Makuda baadae ulikuwa kweli ni usajili wenye tija . Mchezaji anachukuliwa timu fulani kuja kuleta changamoto ya kiufundi na kukidhi haja ya kocha katika kutengeneza timu ya ushindani. 

Isitoshe mchezaji binafsi anazidi kukuza kipaji chake na kuing'arisha nyota yake kisoka. Miaka imepita badala ya kujifunza ili twende mbele zaidi , ndo kwanza tunaiponda misingi iliyojengwa na makocha kama Tito Mwaluvanda, Mshindo Msolwa, Popadic, Shungu na James Siang'a. 

Hao ni baadhi ya makocha wazawa na wageni ambao walikataa siasa katika soka na kufanya usajili ambao ulileta faida kwa timu na mchezaji binafsi. 

Mwamba Kizota anatolewa Tindo ya Tabora na kutua Jangwani hakuna aliyekuwa aliyejua utajiri wa kipaji kilichokuwa ndani ya mtu yule ambaye kwa sasa, kapumzika usingizi wa milele pale kisutu. Hussein Aman Marsha toka Pamba, Pawasa, Akili Mali, Tegete, Makoye wote hao toka Makongo usajili wao uliacha kumbukumbu nzuri kwa klabu na mchezaji binafsi. 

Sasa leo usajili una taswira nyingi sana, kukomoana bila kujali kipaji cha mchezaji wala masilahi ya klabu, kusajili kwa masilahi binafsi aidha umaarufu au mambo ya 10℅ bila kujali mahitaji ya benchi la ufundi. 

Abdi Banda msimu uliopita aligeuka lulu kwa kazi nzuri aliyokuwa akiifanya pale Coastal Union kama beki wa kushoto. Ni kijana mdogo na mwenye kipaji haswa na tayari alishaanza kukamata headlines za waandishi wa habari za michezo. 

Ni kweli Simba ilimuhitaji Banda? Kwanza kabisa usajili wake uligubikwa na sintofahamu lakini leo hii Chippo anahaha kutafuta mrithi wa beki huyo wakati Banda pale Msimbazi amegeuka mtazamaji hana uhakika wa namba. Daah hii ndo Tanzania. 

Akida Makunda alikuwa Yanga kuendeleza makali ya Sanifu Lazaro winga ya kulia na hata mkongwe huyo alipoanza kupigwa benchi, tulikuwa tunaona kabisa kwa nini Makunda kasajiliwa na kazi inaonekana. 

Charles Edward Manyama kwa nini atumiki kwa zaidi ya 60% wakati umemsajili kutokana na mapungufu mengi ya Oscar Joshua? Au Charles sio mbadala sahihi wa Oscar? Tunaua vipaji vya wanandinga wetu mapema bila kujijua. 

Ulimrudisha Omega Seme wa nini kutoka Prisons wakati humtumia hata kwa 30℅ ? Wakati Prisons wanamlilia usiku na mchana? Ni kweli Chanongo kaisha hivyo mpaka aonekane hana umuhimu? Kiemba je? 

Kuna maswali mengi unaweza jiuliza na mwisho wa siku ukakosa majibu. Usajili wa ligi kuu kwa sasa ni zaidi ya Escrow kwenye siasa. Ni kudumaza vipaji vya wachezaji , timu na soka kitaifa. Samuel Samuel - 0652464525

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!