Uingereza kugomea Kombe la Dunia-2018
Na Oscar Oscar Jr
Mwenyekiti wa zamani wa chama cha soka nchini Uingereza, FA, David Bernstein ameibuka na kusema kuwa, ni bora mataifa ya Ulaya yakagomea michuano ya kombe la Dunia ambayo imepangwa kufanyika 2018 nchini Urusi, mpaka pale shirikisho la soka la kimataifa, FIFA litakapofanyiwa mabadiliko makubwa katika utendaji.
Mwenyekiti huyo wa FA wa zamani amesema, England peke yake haiweza kugomea kwa sababu inaweza kujiweka kwenye mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kufungiwa kwenye michuano hiyo lakini kama mataifa yote ya Ulaya yatashirikiana kuna uwezekano jambo hilo likafanikiwa.
David ameendelea kusema kuwa, FIFA imekuwa chombo ambacho kimegubikwa na mambo mengi yasiyostahili na kitendo cha Rais wa FIFA, Sepp Blatter kugombea tena kwa mara ya tano mfululizo ni ishara tosha kuwa, mchezo wa soka utaendelea kuongozwa kwenye mazingira ambayo sio halali.
Madai hayo ya Kugomea michuano ya kombe la Dunia 2018, yameibuka baada ya siku ya Alhamisi ya wiki iliyopita kamati ya maadili na sheria ya FIFA, kutoa ripoti ambayo haielezi kukiukwa kwa sheria za soka kwa kitendo cha Urusi kupewa uenyeji wa michuano hiyo mikubwa Duniani 2018, huku Quatar wao wakipewa kuandaa mwaka 2022.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa zamani wa FA, hakuna sababu za msingi kwa mataifa ya Ulaya na mahali pengine duniani kuendelea kuongozwa na viongozi ambao wamejaa rushwa na kufanya baadhi ya watu kukosa haki zao.
0 comments:
Post a Comment