Kengele ya hatari yaanza kulia kwenye kibarua cha Maximo
Na Samuel Samuel
Yanga SC mabingwa wa nchi hii kwa mara 24 jumamosi hii watakuwa mkoani Shinyanga kuwavaa wageni wa ligi Stand United katika uwanja wa Kambarage. Timu zote zinakutana zikiwa na kumbukumbu ya kutoa sare tasa .
Yanga ilidroo na Simba huku Stand United, waliwagomea wakongwe wa ligi kuu timu ya Kagera Sugar nyumbani kwao mjini Kagera.
Stand United ina pointi tano kwenye msimamo wa ligi ilihali yanga wana pointi saba. Wakati Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar katika mechi ya ufunguzi, nao Stand United walinyukwa 4-1 na wageni wenzao wa ligi timu ya Ndanda FC katika uwanja wa Kambarage.
Maximo atake asitake ni lazima ashinde mechi hiyo kuondoa sitofahamu iliyoaanza kujijenga kwenye kibarua chake. Baada ya mechi ya juzi dhidi ya Simba, mashabiki wa timu hiyo inayotokea mitaa ya Twiga na Jangwani wamegawanyika pande mbili.
Wapo wanaosadiki kocha huyo apewe nafasi zaidi lakini wenye nyoyo nyepesi washaanza kumnyooshea mkono wa kwaheri. Maximo analaumiwa kuwatumia Jaja na Coutinho ambao toka ligi ianze hawajaonesha mchango wowote kuisaidia timu hiyo kupata ushindi.
Mashabiki wa timu hiyo wanataka kuona Maximo akiwapa nafasi mafowadi kama, Kiiza, Javu, Tegete na kumpanga winga ya kushoto Nizar Khalfan ili Saimoni Msuva abaki winga ya kulia kuipa kasi timu hiyo eneo la fowadi. Stand sio wa kubeza hata kidogo.
Wanakumbukwa kuinyima ushindi Simba SC ndani ya uwanja wa taifa na pia kuwagonga 1-0 Mgambo JKT ndani ya Mkwakwani .
Timu hiyo iliyopanda ligi mwaka huu inatumia mfumo wa 4-4-2 wakati Yanga haitabiriki mpaka sasa imejikita katika mfumo gani baada ya kutumia zaidi ya mifumo mitatu katika mechi zake zote nne iliyocheza mpaka sasa.
Kiufupi tunaweza sema Stand United imebeba tumaini la mbrazil huyo kuendelea kuinoa klabu hiyo kongwe nchini endapo atapata ushindi ndani ya dimba la Kambarage na kuondoa hisia mbaya zinazoanza kumzunguka.
0 comments:
Post a Comment