Uchambuzi: Roma vs Bayern Munich
Na Chikoti Cico.
Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajiwa kushika kasi tena Jumanne ya wiki hii huku moja ya mechi inayosubiriwa kwa hamu ni ya kundi E kati ya Roma dhidi ya Bayern Munich, mechi itakayopigwa jijini Roma, Italia kwenye uwanja wa Stadio Olimpico.
Mpaka sasa Roma ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E ikiwa na alama nne ilizopata kwa kuifunga CSKA Moscow kwa magoli 5-1 na kutoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Manchester City hivyo kama Roma atamfunga Bayern, ataweza kuongoza kundi E na kujitengenezea mazingira mazuri ya kuvuka kwenda hatua ya mtoano.
Kocha wa Roma Rudi Garcia anaweza kumkosa kiungo Seydou Keita ambaye hakucheza kwenye mechi ya ligi dhidi ya Chievo baada ya kuumia wakati akiichezea Mali kwenye mechi za kimataifa.
Wakati huo huo, katika mechi tano zilizopita katika ligi ya Serie A na ligi ya mabingwa Ulaya Roma wameshinda michezo mitatu, wamefungwa mchezo mmoja na kutoka sare mchezo mmoja.
Kikosi cha Roma kinaweza kuwa hivi: Skorupski; Maicon, Manolas, Yanga-Mbiwa, Cole; Pjanic, Nainggolan; Gervinho, Totti, Florenzi; Destro.
Kwa upande wa Bayern Munich kocha Pep Guadiola atatamani kuendeleza rekodi nzuri ya kutokufungwa mpaka sasa kwenye msimamo wa kundi E ambako Bayern wanaongoza wakiwa wamejikusanyia alama sita baada ya kuzifunga Manchester City na CSKA Moscow wote kwa goli 1-0.
Kiungo wa Bayern Munich Frank Ribery anaweza kuanza kwenye mechi hiyo baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi lakini Bayern watawakosa Kipa Pepe Reina na kiungo Thiago Alcantara ambao bado ni majeruhi.
Takwimu zinaonyesha mpaka sasa Bayern wameshinda michezo yote mitano iliyopita kwenye mechi walizocheza katika ligi ya Bundesliga na ligi ya mabingwa Ulaya.
Kikosi cha Bayern Munich kinaweza kuwa hivi: Neuer; Alaba, Boateng, Dante, Bernat; Lahm, Alonso; Ribery, Robben, Muller; Lewandowski.
Msimu wa ligi ya Mabingwa Ulaya wa mwaka 2010/2011 Roma na Bayern walikutana kwenye hatua ya makundi na Bayern kushinda mechi ya kwanza kwa magoli 2-0 huku Roma ikishinda mechi ya marejeano kwa magoli 3-2
0 comments:
Post a Comment