Searching...
Image and video hosting by TinyPic
7 August 2015
Friday, August 07, 2015

Uhalisia wa soka letu na Gereza la makuti.


Na Martin Kiyumbi.
Kutumia kipaji chako haimaanishi hutokuwa na matatizo kadri siku zinavyokwenda. Utakutana nayo na wote huwa tunakutana nayo. Hatima yetu huwa inategemea jinsi tunavyoyachukulia matatizo hayo . Binadamu siku zote huwa tunachukulia Matatizo yetu kwa aina mbili , ya kwanza kama vizuizi na ya pili kama viunzi . 
Kipindi tunapoamua kuyachukulia matatizo kama vizuizi huwa hatufanyi juhudi zozote za kujitoa . Huwa Tunaishia kushusha pumzi na kusema "Haiwezekani, Matatizo haya yatatukwamisha tu ". Kuna utofauti mkubwa sana tunapoamua kuchukulia matatizo yetu kama kiunzi , kwani huwa tumejaa roho ya kuamini kuwa tunaweza kuruka .
Leo hii tuko mwezi wa nane , Mwezi ambao ukikaa kwa umakini utaona tofauti ya kizuizi na kiunzi. Mwezi ambao tulikuwa tunausubiri kwa hamu ili twende utumwani. Mwezi ambao tumejiaminisha sote utumwani kuna maisha bora kuliko nyumbani kwetu.  
Nimiezi kumi ambayo tutashuhudia malalamiko mengi kutoka kwa viongozi wa TFF ya kwamba vijana wengi wanapenda kuangalia Mechi ya Westham United na Manchester City kuliko mechi ya Mbeya City na Mghambo JKT, Ilihali viongozi hao hawajaandaa mazingira mazuri ya kuwafanya vijana wajivunie vya kwao kuliko vya utumwani.
Katika mwelekeo wowote tutakaochagua , tukiweza kuona kwamba kila kiunzi tutakachokiruka kinatuimarisha zaidi na kutuandaa kwa ajili ya kiunzi kinachofuata basi tayari tutakuwa tunaelekea kwenye mafanikio. Lakini kama viongozi wa TFF na bodi ya ligi watatumia ile ya hali ya watu kupenda utumwani kuliko nyumbani kama kizuizi bila kufanya juhudi zozote mahususi na kubaki kusema "Haiwezekani kuwafanya watu wachukie utumwani na kupenda nyumbani " Basi tatizo hili halitokwisha.
Tunatakiwa tuboreshe kwetu, tuchimbe msingi mwingine bora na imara pembeni ya nyumba yetu isiyo vutia. Msingi ambao utasimamisha Ukuta bora na imara wenye matofali bora na imara. Tuachane na habari za kuezeka paa zuri kwenye nyumba ya makuti. Kufanya hivo hatutotofautiana na watu wanaopenda kujifunza kwa juu juu maana watu kama hawa hutaka kufaulu mitihani lakini wanakuwa hawajui kitu. 
Watu wanaojifunza kwa kina huwa wanagundua kuwa elimu waliyoipata huingia katika damu yao. Hujielewa vizuri zaidi wao wenyewe pamoja na ulimwengu wao .Huwa wanaendelea kujenga ujuzi uliokwisha kupatikana kwa kuongeza ujuzi mpya. 
Ujuzi utakaowezesha ligi yetu kuwa bidhaa bora nchini, Afrika na Duniani kwa ujumla. Ujuzi utakaowezesha ligi yetu igombaniwe na wanunuzi wengi wenye bei bora. Ligi itakayoonesha yanayoongelewa kwenye magazeti kuonekana uwanjani. 
Ujuzi utakaowezesha watu kutokusikia Mchezaji analala mzungu wa nne na mchezaji mwenzake, ilihali kule utumwani mchezaji hulala kwenye chumba kizuri, chumba kinachomwezesha aamke asubuhi bila kutoa malalamiko ya mbavu zake kuumia. 
Ujuzi ambao utawezesha timu kuwa na vyanzo vingi vya mapato ili kuviweka karibu na mashabiki, tofauti na sasa ukaribu wa vilabu vyetu na mashabiki ni kwenye viingilio vya mechi. Wakati utumwani huwa wanatuweka karibu kwa kuletewa jezi na viatu vya kina Angel Di Maria tena vyenye saini yake.
Unapofanya jambo lolote la udanganyifu ni lazima ufanye jambo lingine la udanganyifu ili kuficha lile la kwanza na mwisho wa siku maisha yako yatakuwa magumu. Ndiyo maana Watanzania wamechoka kudanganywa kila siku kupewa sukari mwisho wa siku hukomea kupewa maji ya miwa . 
Ukiwa mwaminifu huna haja ya kukumbuka ulisema nini siku za nyuma , ndiyo maana wenye usukani wa gari letu la soka huja na kauli tamu tena mpya kila siku bila kutimiza kauli zile za zamani ambazo huwa bado hazijaisha utamu , hii yote ni kwa sababu hawajawa waaminifu kwetu hata siku moja ndiyo maana watu wengi wameamua kwenda utumwani wakiamini kabisaaa kule utumwani kuna viongozi wa kweli na wenye weredi wa hali ya juu, wenye uwezo wa kushika usukani wa soka kwa ustadi wa hali ya juu bila kutusababishia makovu yoyote yatokanayo na ajali. 
Kiukweli Mioyo ya watanzania wengi ina viraka vingi na kila sehemu unapogusa mioyoni mwao kuna makovu mengi waliyoachiwa. Hii yote ni kutokana na kutokupata wanachotarajia kutoka kwenye mapenzi waliyonayo kwenye soka la nyumbani . 
Kila siku wameishia kulizwa na mpenzi wao soka, hakuna siku waliyopata angalau kutabasamu ukiachana na kupata furaha kitu ambacho kimegeuka kutoka kwenye matamanio kuwa ndoto isiyoweza kufikiwa kwa wakati huu.
Kitu hiki kimewafanya kuwa watumwa tena waliofungwa kwenye gereza la makuti bila mlinzi yoyote. Gereza ambalo waweza kulibomoa hata kwa kidole chako, lakini kutokana na furaha kubwa sana wanayoipata kwenye Gereza hili la Makuti tena lisilo kuwa na walinzi , hawaoni haja ya kulibomoa na kutoroka .
Tusubirini kupelekwa utumwani tukaishi kwenye Gereza la Makuti kuanzia tarehe 08/08 siku ya kuzaliwa kwangu .
ASANTENI.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!