Uchambuzi: Spurs vs Arsenal
Na Oscar Oscar Jr
Leo mchana katika dimba la White Hate Lane utapigwa mchezo wa ligi kuu Uingereza ambapo Spurs watawakaribisha majirani zao, timu ya Arsenal kwenye muendelezo wa ligi kuu Uingereza. Huu ni mchezo unaovuta hisia za wadau wengi wa soka kwa namna mbili tofauti.
Kwanza timu hizi zimekuwa na upinzani wa jadi na tangu mwaka 2007, Arsenal wameshinda ugenini mara moja pekee na pili, kwa mara nyingine timu hizi zinakutana huku zikiwa kwenye ubora wa hali ya juu bila kusahau mbio za kuwania kumaliza msimu ndani ya nne bora ili kupata nafasi ya kucheza klabu bingwa Ulaya.
Leo ni siku nyingine ya kupima ubora wa kiungo Francis Coquelin baada ya kuonyesha kiwango bora siku za hivi karibuni kama kiungo mkabaji hususani kwenye mchezo dhidi ya Manchester City ambao Gunners walishinda kwa mabao 2-0. Kwa nini unatakiwa kumtazama Francis?
Kiungo huyu amekuwa habari ya mjini kwa kulinda vizuri safu ya ulinzi ya Arsenal huku akikaba bila hata kucheza rafu. Kocha wa Spurs, Mouricio Pochettino amekuwa akimtumia Moussa Dembele kama namba 10 na ubora wa kiungo huyo raia wa Ubelgiji umezidi kushika kasi.
Anajua kukaa na mpira mguuni, anajua kupiga chenga za maudhi na mara kadhaa amekuwa akifanyiwa madhambi na mabeki wengi ambazo zimekuwa zikigeuka magoli baada ya Christian Eriksen kuibuka kuwa moja wa wafungaji bora wa mipira hiyo ya kutenga.
Safu ya kiungo ya Spurs huenda ikaanza na mtoto wa nyumbani Ryan Mason na Nabili Bentaleb ambaye alikuwa AFCON na Algeria. Hili ni eneo lingine ambao litakuwa na upinzani mkubwa kutokana na ubora wa Santi Carzola na Mesut Ozil ambaye huenda akawa anatokea pembeni na kupishan na Carzola pale timu itakapokuwa inashambulia.
Safu ya ulinzi ya Gunners itakuwa na shughuli pevu hasa ukizingatia kuwa Nacer Chadli, Andros Townsend, Eriksen na Harry Kane wamekuwa moto wa kuotea mbali.
Kane ambaye amefunga mabao 20 msimu huu kwenye mashindano yote, amegeuza ghafla kuwa moja ya washambuliaji hatari Uingereza na angependa kuonyesha ubabe kwenye mchezo huu dhidi ya Arsenal ambao wamewahi kuwa naye kwenye Akademi yao.
Moja kati ya matatizo makubwa ya Arsenal kwa misimu ya hivi karibuni, ni kukosa muendelezo mzuri wa ushindi katika michezo yao lakini, msimu huu wameonekana kubadilika. Katika mechi tano za hivi karibuni wameshinda zote huku wakifunga mabao 15 na ukuta wao kuruhusu mabao mawili pekee.
Alexies Sanchez na Alex Oxlad Chamberlain huenda wakaukota mchezo wa leo lakini uwepo wa Theo Walcott na Mesut Ozil, unafanya Arsenal kuwa na watu sahihi wa kuziba nafasi hizo.
Kwa upande wa makocha, Arsenal Wenger bado hajawahi kupoteza mchezo wowote anapokutana na kocha Mouricio Pochettino.
Kma Pochettino ataamua kucheza washambuliaji wawili, ni wazi kuwa Emmanuel Adebayor atapata nafasi ya kuwasambaratisha tena Arsenal kutokana na rekodi yake nzuri ya kuwafunga Gunners na kama hilo litatokea, huenda Star huyo wa Togo akarejesha mahusiano mazuri na mashabiki wake wa Spurs ambao wamekuwa wakimzomea ndani ya siku za hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment