Burussia Dortmund yarudi kwenye chati.
Na Oscar Oscar Jr
Baada ya klabu ya Borussia Dortmund kumaliza kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Ujerumani msimu uliopita huku Bayern Munich wakiibuka mabingwa wa Bundesliga, mambo hayakuanza vema kwa upande wao msimu huu.
Mambo yalikuwa mabaya sana kwa upande wao mpaka kufikia hatua ya kuburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo huku baadhi ya wataalamu wa soka wakianza kutilia shaka kuwa huenda timu hiyo ikashuka daraja msimu huu.
Jana wamepata ushindi kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwachapa FSV Mainz kwa bao 4-2 huku mechi iliyopita wakiwachapa Freinburg kwa mabao 3-0 na hii ni ishara kuwa Dortmund wameanza kurejea kwenye ubora wao.
Katika mchezo huo, Dortmund walipiga mashuti 21 huku 10 kati ya hayo yakilenga lango. Marco Reus ambaye hivi karibuni alisaini mkataba mpya, alifunga bao moja na kupiga pasi moja ya mwisho.
Mabao mengine ya Borussia Dortmund yalifungwa na Subotic, Aubameyang na Nuri Sahin huku yale ya Mainz yakifungwa na Soto na Malli. Vijana hao wa manjano na nyeusi, wamefika kwenye nafasi ya 14 kwenye msimamo na kuondoka mkiani wakiwa na pointi 22.
Wiki ijayo Borussia Dortmund watakwenda kupambana na timu ya VFB Stuttgart ambayo inakamata mkia kwa sasa kabla ya kwenda kucheza ugenini na Juventus kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya klabu bingwa Ulaya.
0 comments:
Post a Comment